Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Wasomi Waishukia Ripoti ya UNESCO, WWF

Na. Mwandishi Maalum.  

Serikali ya Tanzania inatakiwa kuchukua hatua madhubuti za ujenzi wa vyanzo vipya vya uzalishaji wa umeme wa uhakika ili iepuka kushindwa kufikia malengo ya kuwa taifa lenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Sambamba na hilo, Tanzania inatakiwa kuwa na vyanzo vipya vya umeme wa uhakika ili kuepuka hatari ya maeneo ya misitu kugeuka jangwa na kuepuka athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.

Hayo yamebainishwa katika ripoti maalumu ya marafiki wa mazingira waliofanya utafiti kuhusu faida na hasara za ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa Rufiji unaofahamika zaidi kwa jina la Stiegler’s Gorge Hydropower Project unaotekelezwa katika eneo la hifadhi la Selous.

Ripoti hiyo ya kitaalamu ambayo inatarajiwa kuzunduliwa hivi karibuni imeandaliwa na wataalamu wabobezi watano wa mazingira,uhifadhi na uchumi hapa nchini na imechambua upinzani wa ndani na wa kimataifa kuhusu ujenzi wa mradi wa Stiegler’s Gorge na hasa hoja zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori (WWF) za kupinga mradi huo usitekelezwe.

Mmoja wa wajumbe wa jopo hilo la wataalamu, Dk. Abubakar Rajabu katika mahojiano mafupi na waandishi wa habari yaliyofanyika jana jijini Dar es Salaam alisema yeye na wataalamu wenzake wamefanya utafiti wa kina na wa kitalaamu na kugundua kuwa upinzani unaoonyeshwa na mashirika hayo ya kimataifa dhidi ya ujenzi wa mradi huo umejikita zaidi katika hoja za upotoshaji ambazo lengo lake ni kutaka Tanzania iendelee kudumaa kiuchumi na kuharibu eneo la misitu kutokana na shughuli za kibinadamu.

Dk Rajabu alisema katika utafiti wao wamebaini kuwa Tanzania ipo hatarini kugeuka jangwa na pia kukumbwa na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi kutokana na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na shughuli za kibinadamu na hasa ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa na ili kuepuka hali hiyo ni lazima kutafuta njia mbadala aliyoitaja kuwa ni umeme wa uhakika na nafuu.

Aidha, alisema ili Tanzania iweze kufikia malengo yake ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, serikali inalazimika kujenga vyanzo vipya vya umeme wa uhakika na rahisi ili kuziwezesha sekta nyeti za Viwanda, Kilimo na Madini kukua kwa kasi.

“Serikali iko katika vita ya kiuchumi, vita hii si ya lelemama na kimsingi ni vita ya kila Mtanzania hivyo wote tuko kwenye vita hii. Sisi kama watalaamu kwenye mambo ya uhifadhi na mazingira tulipoona ripoti za UNESCO na WWF zilizokuwa zikipinga ujenzi wa mradi wa Stiegler’s Gorge ambao tulikusudia kuutekeleza tangu miaka ya 60 na tunajua manufaa yake tuliona tusipuuze utafiti wa wenzetu hawa, hebu tujiridhishe na hoja zao.

“Mimi na wenzangu tukaingia kazini, tulifanyia kazi hoja zao zote na tulichogundua ni kwamba hoja zao ZOTE za kupinga mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa Rufiji hazina ushahidi wa kutosha wa kisayansi bali upinzani huu lengo lake ni kutaka kuifanya Tanzania isipige hatua kimaendeleo, tuendelee kudumaa kiuchumi na katika nyanja zote muhimu. Lakini jambo kubwa kabisa tulilogundua ni hawa wenzetu wanataka miaka michache ijayo sehemu kubwa ya nchi yetu igeuke kuwa jangwa kwa sababu ya ukataji miti na hilo kwa ujumla litaharibu kabisa mazingira na kuifanya Tanzania kutofikia azma yake ya kuwa nchi ya uchumi wa kati na kuwarudisha nyuma watanzania kimaendeleo na Taifa liendelee kuwa tegemezi na pengine kutoweka kabisa katika ramani ya dunia:. Vyanzo vya maji vitakauka yote; mvua zitakuwa za kusadikika, kilimo kitadumaa, wanyama na ndege watakwisha wote, utalii hautakuwepo tena, viwanda vitayeyuka, ajira zitakuwa hadithi, mardhi na utapiamlo ndio itakuwa habari ya kila siku, nguvu kazi itapotea na Taifa litakuwa tegemezi nakadhalika. Na hayo yote yatachangia kuzorota kwa usalama wa taifa na nchi inaweza kutotawalika”.

“Niwape kidogo tu tulichogundua katika utafiti kwa sababu mengi mtayapata kwenye uzinduzi wa ripoti na mimi sitaki kumaliza uhondo, ni kwamba Tanzania ina eneo la misitu lenye kilomita za mraba 35,254 na kila mwaka eneo la misitu lipatalo kilomita za mraba 412 linateketezwa kwa ajili ya mkaa na kuni, ambacho ndio chanzo kikuu cha nishati kwa zaidi ya asilimia 85 ya watanzania wote. Kwa hiyo endapo hapatakuwa na nishati mbadala zaidi ya umeme na gasi, safari ya Tanzania kuelekea katika HATARI YA KUTOWEKA KATIKA RAMANI YA DUNIA ingekuwa imeanza rasmi, kama sio upeo mpana wa utawala kuona mbali na kuamua kutekeleza mradi mkubwa wa kufua umeme wa Rufiji.  mpaka hapo nadhani mnaona hatari inayotunyemelea.

“Lakini pia, katika utafiti wetu tumegundua kuwa asilimia 45 ya wafanyabiashara hapa Nchini wanamiliki jenereta ambazo zinatumia mafuta ya dizeli, moshi unaotokana na dizeli unachafua sana mazingira na hutuwezi kupiga hatua kiviwanda kama uzalishaji wetu utakuwa unategemea jenereta na hivyo kufanya gharama ya uzalishaji kuwa kubwa na hivyo kuongeza ughali wa maisha. Hivyo ni lazima tuwe na umeme wa uhakika alisema Dk Rajabu.

Alisema ripoti inakuja kukata kiu ya maswali na kuondoa mashaka ya aina yoyote kuhusu utekelezaji wa mradi huo na umuhimu wa taifa kuwa na umeme wa uhakika na imeangalia nyanja zote zilizo tajwa kuwa na shaka na kupata ukweli wake.

Alisisitiza kuwa hoja za kupinga mradi wa Stiegler’s Gorge zilizotolewa na wapinzani wa ndani na nje baada ya kuchujwa kisayansi zimekosa nguvu na hasa ikizingatiwa kuwa eneo la Selous lenye kilomita za mraba 50,000 ni pungufu ya asilimia mbili tu ndilo linalotumika kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa maji wa Rufiji.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama