Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Washiriki wa  Mafunzo  ya  WISN na POA Watakiwa  Kutoa Huduma Bora Kwa Wananchi

Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Utawala na Rasilimaliwatu Mkoa wa Katavi Bi. Crescencia Joseph akifunga mafunzo ya mifumo  ya WISN na POA, Mifumo  hiyo inatumika kubaini mahitaji ya watumishi katika vituo vya kutolea huduma za afya na vipaumbele katika kuwapangia watumishi hao vituo vya kazi , mafunzo hayo yanayowashirikisha makatibu wa afya,maafisa utumishi,wataalamu wa takwimu za afya na waganga wakuu wa Wilaya za mkoa wa Katavi jana Jijini Mbeya.

Frank Mvungi- MAELEZO,  Mbeya

Washiriki wa mafunzo ya mfumo unaotumika kubaini mahitaji ya watumishi katika vituo vya kutolea huduma za afya (WISN) na ule unaotumika kupanga mgawanyo wa watumishi hao kulingana na uhitaji wa kila kituo (POA) wametakiwa kuwa chachu ya kutoa huduma bora kwa wananchi.

Akizungumza jana, Jijini Mbeya wakati akifunga mafunzo kwa makatibu wa afya, maafisa utumishi, wataalamu wa takwimu za afya, na waganga wakuu wa Wilaya wa mkoa wa Katavi, Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Utawala na Rasilimaliwatu wa mkoa huo, Bi. Crescencia Joseph, amesema kuwa washiriki wa mafunzo hayo wamejengewa uwezo ili waweze kutumia mifumo hiyo iliyorahisishwa kuwapangia vituo vya kazi watumishi wapya, na katika kuomba watumishi wapya kulingana na mahitaji.

 Mifumo hii miwili iko chini ya  Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), pamoja na Ofisi ya Rais – Utumishi, kwa kushirikiana na Mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID).  Mradi huu wa miaka mitano unatekelezwa katika mikoa 13 ya Tanzania bara.

’’ Washiriki mmeonyesha kuwa mtazingatia maadili ya utendaji kazi wenu wa kila siku kwani  mmepewa dhamana hii na Serikali ili muweze kuwahudumia wananchi katika halmashauri  za Mkoa wa Katavi hasa katika kuimarisha huduma za afya”. Alisisitiza  Bi. Crescencia.

Akifafanua Bi. Crescencia amesema  kuwa  Serikali inamatarajio makubwa kutoka kwa washiriki wa mafunzo hayo katika kuimarisha huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma kwa kuwa huo ndio msingi na Dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano inayosisitiza katika kutoa huduma bora kwa wananchi hasa wale wanyonge.

 Mifumo ya WISN na POA iko chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na Ofisi ya Rais Utumishi, ikiwa ni moja ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kuboresha huduma za afya hapa nchini.

 


FacebooktwittermailFacebooktwittermail