Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Wanawake Milioni 2.6 Kunufaika na Mradi wa ‘50 Million Women Speak Project’

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bw. Julius Mbilinyi akifungua kikao cha wadau wa Kitaifa wa masuala ya maendeleo ya wanawake nchini kilichofanyika jijini Dodoma.Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Sekta ya Jamii kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mary Makoffu na Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Vijana na Uwezeshaji Kiuchumi, Esther Riwa.

Na Jacquiline Mrisho.

Takribani wanawake milioni 2.6 wanategemea kunufaika na mradi ujulikanao kama 50 Million Women Speak Project’ unaolenga kuwawezesha wanawake kupata taarifa za kiuchumi kupitia mtandao wa mawasiliano.

Takwimu hizo zimetolewa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bw. Julius Mbilinyi alipokuwa akifungua kikao cha wadau wa Kitaifa wa masuala ya maendeleo ya wanawake nchini.

Bw. Mbilinyi amesema kuwa takwimu za Hali ya Afya na Demografia za mwaka 2015 zinaonesha  asilimia 51 ya Watanzania ni wanawake ambao kati ya wanawake hao, asilimia 70 wanajihusisha na shughuli za kilimo na ujasiriamali hivyo mradi huo utatumika kusaidia kuimarisha shughuli zao.

Msimamizi wa Mradi huo kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bw. Wilson Muyenzi akitoa mada katika kikao cha wadau wa Kitaifa wa masuala ya maendeleo ya wanawake nchini kilichofanyika jijini Dodoma.

“Mradi huu wa miaka mitatu unategemea kunufaisha wanawake kutoka nchi 30 za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi pamoja na Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika ambazo kwa ujumla zinakadiriwa kuwa na wanawake milioni 500, kwa Tanzania mradi huu unategemea kunufaisha takriban wanawake milioni 2.6.” alisema Bw. Mbilinyi.

Bw. Mbilinyi ameongeza kuwa mradi huo una umuhimu kwa kuwa utawafikia wanawake hasa wa vijijini ili kuwawezesha kujiletea maendeleo jumuishi yanayoenda sawa na utekelezaji wa malengo endelevu ya Kimataifa, mpango wa miaka mitano ya maendeleo, Agenda ya Afrika Tuitakayo pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo.

Vile vile mradi huo utawezesha wanawake kunufaika kwa kupata taarifa mbalimbali za kibiashara zikiwemo za upatikanaji wa mitaji, masoko na stadi za biashara kwa kutumia mitandao ya mawasiliano, vituo vya taarifa za wanawake, majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi pamoja na vikundi mlezi.

Wadau wa masuala ya maendeleo ya wanawake nchini wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumaliza kikao cha kujadili kuhusu mradi ujulikanao kama 50 Million Women Speak Project’ unaolenga kuwawezesha wanawake kupata taarifa za kiuchumi kupitia mtandao wa mawasiliano kilichofanyika jijini Dodoma.

Akizungumzia mkutano huo, Bw. Mbilinyi amesema kuwa wamemua kufanya kikao cha wadau wa maendeleo ya wanawake takribani 50 ili kuwafahamisha kuhusu mradi huo, jinsi utakavyofanya kazi pamoja na kukusanya mawazo yao yatakayosaidia kuboresha utekelezaji wake nchini.

Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi huo kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bw. Wilson Muyenzi amesema  kuwa mradi huo unategemewa kuongeza fursa za ajira kwa wanawake, kufahamu gharama za ubadilishaji fedha pamoja na kupanua masoko kwenye nchi mbalimbali zinazoshiriki katika mradi huo.

“Wanawake watakaotumia huduma za mradi huu wataweza  kuongeza mapato yao kwa kiasi cha dola 50,000 hadi 100,000 kwa kipindi cha miaka mitatu ya utekelezaji wa mradi pamoja na kuongeza ajira kwa vijana wanawake kwa asilimia 10.” Alisema Bw. Muyenzi.

 

121 thoughts on “Wanawake Milioni 2.6 Kunufaika na Mradi wa ‘50 Million Women Speak Project’

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *