Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Wananchi Watakiwa Kutoa Taarifa Hospitali Zinazotoza Mama Wajawazito

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, DODOMA

Serikali imewataka wananchi kutoa taarifa kuhusu hospitali zinazotoza fedha kwa ajili ya matibabu kwa akina mama wajawazito ili kuweza kuchukua hatua muhimu kukomesha hali hiyo.

Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu  Hawa Chakoma lililohusu matibabu bure kwa mama wajawazito.

Dkt. Ngugulile amesema kuwa mama wajawazito ni moja ya makundi maalumu wanaostahili kupata huduma za matibabu bure kama ilivyooneshwa katika mwongozo na uchangiaji wa huduma za afya wa mwaka 1997.

“Mwongozo umeweka bayana kuwa kina mama wajawazito ni haki yao kupewa huduma zote bila malipo na sio zile tuu zinazohusu huduma za ujauzito katika mwongozo uliopitiwa mwaka 2009/2010 imetamkwa bayana kuwa huduma za afya kwa mama wajawazito ni bure, ikiwa na maana kwamba mara tu mwanamke anapokuwa na ujauzito huduma zote kuanzia kliniki ya wajawazito, pale anapogundulika maradhi yoyote, pamoja na huduma ya kujifungua sanjali na kumuona daktari, kupatiwa vipimo, kupewa dawa na kufanyiwa upasuaji pale inapohitajika kufanya hivyo” amefafanua Dkt. Ndugulile.

Aidha, Dkt. Ndugulile amesema kuwa Wizara imeanzisha utaratibu wa kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vinavyohitajika wakati wa kujifungua ambapo watapewa akina mama wajawazito wanapokaribia kujifungua.

Hata hivyo, Dkt Ndugulile amesema kuwa kwa sasa kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa akina mama kujifungua katika vituo vya afya ambapo zaidi ya asilimia 60 ya akinamama wanajifungulia kwenye vituo vya afya.

Mbali na hayo, Serikali imezitaka Halmashauri zote nchini kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sera hiyo ili akina mama wajawazito wapate huduma za matibabu bure kama Mwongozo wa Uchangiaji wa mwaka 1997 na Sera ya Afya ya mwaka 2007 inavyoelekeza.


FacebooktwittermailFacebooktwittermail