Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Wananchi Waelezwa Watakavyonufaika na Mradi Mpya Wa Umeme

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akizungumza na wananchi wa PembaMnazi, Kigamboni jijini Dar es Salaam; alipofanya ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, Julai 3, 2018.

Na Veronica Simba – Dar es Salaam

Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu amefanya ziara katika Wilaya ya Kigamboni, mkoani Dar es Salaam na kuwaelezea wananchi wa eneo hilo watakavyonufaika na Mradi mpya wa umeme unaoitwa Peri-Urban.

Alifanya ziara hiyo jana, Julai 3, 2018 akiwa ameambatana na maafisa mbalimbali kutoka wizarani, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Akizungumzia mradi huo mpya, Naibu Waziri alisema kuwa Serikali imeuanzisha mradi huo mahsusi kwa lengo la kupeleka umeme katika maeneo yanayokua kwa kasi.

“Kutokana na kasi ya ukuaji wa maeneo mbalimbali, ikiwemo Kigamboni, kumekuwepo na ongezeko la uhitaji wa viwanda pamoja na mahitaji mengine ya wananchi. Hivyo Serikali imeonelea vema kuanzisha Mradi huu mpya maalum kwa ajili ya maeneo hayo na utatekelezwa sambamba na miradi mingine ya umeme inayoendelea.”

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (mbele-katikati) akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali wilayani Kigamboni na maafisa kutoka wizarani, TANESCO na REA; wakati wa ziara yake wilayani humo Julai 3, 2018 kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme pamoja na kuzungumza na wananchi.

Ameongeza kuwa mradi huo mpya utazinduliwa hivi karibuni ambapo kazi ya kusambaza umeme itaanza kutekelezwa mwezi Agosti mwaka huu.

“Kinachoendelea kwa sasa ni mchakato wa kufanya tathmini. Mpaka mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu, tutakuwa tumeshamteua Mkandarasi wa kutekeleza miradi hiyo,” alisema.

Naibu Waziri aliwataka wananchi kujiandaa ipasavyo ili Mradi utakapoanza kutekelezwa katika maeneo yao, waweze kuunganishiwa.

Aidha, aliwaasa kuwa makini na matapeli wanaojinadi kufanya kazi TANESCO na kuwatoza malipo zaidi ya yale yaliyoainishwa na Serikali.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu na Ujumbe wake wakiangalia daraja lililokatika katika mtaa wa Tundwi Songani, Kata ya PembaMnazi, Wilaya ya Kigamboni, wakati wa ziara yake kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme, Julai 3, 2018. Hii ni moja ya changamoto ambazo wananchi wa eneo hilo walimwomba awafikishie kwa Waziri husika ili awasaidie.

Awali, akitoa taarifa ya hali ya umeme katika eneo la Kigamboni, kwa Naibu Waziri, Meneja husika wa TANESCO, Mhandisi Hadija AbdalaHemed, alibainisha kuwa, katika kipindi cha mwaka huu wa bajeti, Shirika hilo linatarajia kutekeleza miradi 23 ya kusambaza umeme katika Wilaya ya Kigamboni. Aidha, alisema kuwa, jumla ya vijiji 35 vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa Peri-Urban.

Mradi huo wa kusambaza umeme wa Peri-Urban unatekelezwa katika Mkoa wote wa Pwani pamoja na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Dar es Salaam, ikiwemo Kigamboni.

Katika ziara yake Kigamboni, Naibu Waziri alitembelea na kukagua maendeleo ya Kituo cha kupooza umeme cha Dege, kutembelea na kuzungumza na wananchi wa Mtaa wa Minondo, Gorani, Mwasonga pamoja na Mtaa wa Pemba Mnazi.

54 thoughts on “Wananchi Waelezwa Watakavyonufaika na Mradi Mpya Wa Umeme

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *