Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

TADB Kusaidia Wakulima wa Kanda ya Ziwa

Na Mwandishi wetu,

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imedhamiria na kujizatiti kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa katika  kuleta mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo kwa wakulima wa Kanda ya Ziwa na Tanzania kwa ujumla ili kusaidia upatikanaji wa fedha na sera nzuri zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini.

Dhamira hiyo imewekwa wazi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo, Bibi Rosebud Kurwijila wakati akitembelea miradi mbalimbali ya kilimo mkoani Mwanza hivi karibuni.

Bibi Kurwijila alisema kuwa katika kutekeleza mkakati wa kuwafikia wakulima wengi zaidi nchini TADB imejipanga kutoa huduma kupitia kongane mpya nane ili kuongeza tija kwa wakulima nchini.

“Kongane ni njia ya kimkakati ya kijiografia yenye kujikita katika shughuli za kilimo zinazohusiana, wasambazaji na taasisi zinazohusishwa katika kujenga usawa wa moja kwa moja miongoni mwa wadau ili kukidhi mahitaji ya wakulima nchini, benki ya kilimo itawafikia kupitia njia hii,” alisema.

Aliongeza kuwa kongane ya Kanda ya Ziwa ambayo inajumuisha mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Shinyanga, Geita na Simiyu itatoa fursa ya ushindani kwa njia endelevu ili kuchagiza uhusiano na ushirikiano katika uongezaji wa thamani hasa katika makundi mbalimbali ya minyororo ya thamani pamoja na taasisi na mamlaka za udhibiti zinazosaidia sekta ya kilimo nchini.

Kwa mujibu wa mpango kazi wa Benki hiyo, dhana ya Kongane imeandaliwa kwa kutokana na mgawanyo wa kiokolojia kwenye kilimo kuzingatia kanda zilibainishwa kwenye Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Kilimo (ASDP II 2016/17-2020/21) ambapo mikoa imegawanywa ili kurahisisha utoaji wa huduma na mapendekezo ya teknolojia kwenye mifumo sawa ya uzalishaji. Kongane hizi zimezingatia utendaji wa kila mnyororo wa thamani ya kilimo na faida za linganifu katika kila mkoa katika uzalishaji.

Mpango kazi huo unaweka bayana kuwa matumizi ya Kongane yanalenga kuchagiza ufanisi katika kuimarisha minyororo ya thamani hasa wakati hakuna misingi thabiti katika kuendeleza minyororo hiyo ambayo inajumuisha kuanzia uzalishaji, usindikaji, usafiri, usambazaji, kuwezesha mazingira na soko. Hivyo uhitaji wa kuingilia kati juhudi hizi kutoka kwa wadau wengi ambao hawawezi kutatua suala lolote kwa pekee.

TADB iliyozinduliwa rasmi mnamo tarehe 08 Agosti 2015 imeanzishwa kwa madhumuni makubwa mawili ya kusaidia utoshelezi na usalama wa chakula endelevu nchini Tanzania; na kuchagiza mapinduzi ya kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.


FacebooktwittermailFacebooktwittermail