Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Wakazi 234,398 wa Chalinze kunufaika na mradi wa maji.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa hafla ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa mfumo wa kusafirisha na kusambaza maji safi pamoja na matenki ya kuhifadhi maji katika Jimbo la Chalinze. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Chalinze, Mhandisi Christer Mdomba, kulia ni Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo.

Frank Mvungi.

Takriban wakazi 234,398 wa  Chalinze watanufaika na  mradi wa upanuzi wa mtambo na ujenzi wa mfumo wa kusafirisha na kusambaza maji safi pamoja na matenki ya kuhifadhi unaolenga kuondoa changamoto ya upatikanaji wake katika Jimbo hilo.

Akizungumza  kwa niaba ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa hafla ya kukagua maendeleo ya mradi  huo, Waziri wa Maji na Umwagiliaji,  Mhandisi Gerson Lwenge amesema kuwa Serikali inaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo na kumtaka mkandarasi kuongeza kasi katika kutekeleza mradi huo.

“Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata maji safi na salama ndio maana tumeweka wataalamu wetu hapa kumsimamia mkandarasi ili afanye kazi  kwa ubora na kwa kasi kama ambavyo Waziri Mkuu aliagiza alipotembelea mradi huu mwezi Machi mwaka huu”, alisisitiza Lwenge.

Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa DAWASA, Mhandisi Romanus Mwangingo akitoa maelezo ya utekelezaji wa mradi kusafirisha na kusambaza maji safi pamoja na matenki ya kuhifadhi maji katika Jimbo la Chalinze.

Akifafanua, Mhandisi Lwenge amesema kuwa hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa  mradi huo awamu ya tatu ni ulazaji wa mabomba ya kusafirisha na ya kusambaza maji, ujenzi wa matanki 19, na ujenzi wa  mtambo wa kusafishia maji ambao unaendelea.

Kazi nyingine zinazoendelea katika kutekeleza mradi huo ni ujenzi wa vituo 351 vya kuchotea maji ambapo vituo 27 vimekamilika,vituo 226 vipo katika hatua mbalimbali na vituo 98 havijaanza kujengwa.

Akizungumzia hatua zinazochukuliwa na mkandarasi wa mradi huo, Mhandisi Lwenge amesema kuwa ni kuongezeka kwa upatikanaji wa vifaa kwa wakati katika eneo la mradi, kuongeza wafanyakazi na maeneo ya kazi na kuteua mwakilishi wa kampuni anayeweza kutoa maamuzi kwa niaba ya kampuni inayotekeleza mradi.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo akizungumza wakati wa hafla ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa mfumo wa kusafirisha na kusambaza maji safi kutoka mto Wami pamoja na matenki ya kuhifadhi maji katika Jimbo la Chalinze. Kushoto ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge,kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga.

Moja ya tenki la maji linalojengwa katika chanzo cha maji cha mto Ruvu ikiwa ni sehemu ya mradi huo.

Aidha, Waziri Lwenge amesema kuwa Serikali itatoa ufumbuzi wa changamoto ya wananchi wa Jimbo hilo kulipia malipo ya huduma  (service charge) hata pale wanapokuwa hawajapata huduma hiyo ili kuwe na utaratibu mzuri unaowezesha wananchi kulipia huduma pale wanapotumia tu na si vinginevyo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo hilo, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema yeye binafsi anaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna inavyoshughulikia  changamoto zinazowakabili wananchi wa Jimbo hilo ikiwemo ya maji.

“Naridhika na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya mradi huo ambao ukikamilika utasidia kwa kiwango kikubwa kuondoa changamoto ya upatikanaji wa maji katika jimbo hili hivyo wananchi wataweza kuongeza kasi katika shughuli za maendeleo”, alisisitiza Ridhiwani.

Akifafanua amesema anaunga mkono juhudi za Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo .

Mnamo mwezi Machi mwaka huu, Waziri  Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa alifanya ziara ya kutembelea mradi huo na kukagua shughuli za ujenzi wa miundombinu ya mradi  huo  Awamu ya Tatu na baada ya ziara aliagiza mkandarasi anayetekeleza mradi huo ambaye ni Overseas Infrastracture Alliance (OIA)Pv Ltd kutoka India  mwenye ubia na Kampuni ya Pratibha Industries nayo ya India kukamilisha kazi hiyo ,mkandarasi wa mradi huo ameshalipwa shilingi 38,716,375,627 ikiwa ni asilimia 42 ya gharama ya mradi.

Uhaba wa maji safi na salama umelikumba jimbo la Chalinze kwa kipindi kirefu. Kwa sasa wanaopata huduma ya maji safi na salama ni 220,241, mradi ukikamilika, watakaopata huduma hiyo watafikia jumla ya 234,394.

 

67 thoughts on “Wakazi 234,398 wa Chalinze kunufaika na mradi wa maji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *