Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Waganga Wafawidhi Hakikisheni Wanafunzi Wanaoanza Shule za Bweni Wanafanyiwa Uchunguzi wa TB – Ummy Mwalimu

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto mhe. Ummy Mwalimu akisisitiza jambo wakati akitoa tamko kuhusu maadhimisho ya siku ya Kifua Kikuu Dunia leo mjini Dodoma  yanayotarajiwa kufanyika tarehe 24 machi, 2018.kulia .Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma Dkt. Beatrice Mutayoba na Kushoto ni Mkurugenzi wa huduma za Kinga Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi.

Mkurugenzi wa huduma za Kinga Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi (wakwanza kushoto) akisisitiza mikakati ya Serikali katika kuwashirikisha waganga wa tiba asili katika mapambano dhidi ya ya Kifua Kikuu kuelekea  maadhimisho ya siku ya Kifua Kikuu Dunia yanayotarajiwa kufanyika tarehe 24 machi, 2018. Katikati ni Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto mhe. Ummy Mwalimu.

Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma Dkt. Beatrice Mutayoba  (katikati) akisisitiza jambo mara baada ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto mhe. Ummy Mwalimu kutoa tamko leo mjini Dodoma kuhusu maadhimisho ya siku Kifua Kikuu Dunia yanayotarajiwa kufanyika tarehe 24 machi, 2018.kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari  MAELEZO bi Zamaradi Kawawa, Kushoto Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto mhe. Ummy Mwalimu.

Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia tamko la   Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto mhe. Ummy Mwalimu  leo mjini Dodoma  kuhusu maadhimisho ya siku ya Kifua Kikuu Dunia yanayotarajiwa kufanyika tarehe 24 machi, 2018.

 

Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.

Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amewaagiza Waganga Wafawidhi wa hospitali na vituo vya huduma kuhakikisha wanafunzi wote wanaoanza shule za Bweni wanafanyiwa uchunguzi  wa Kifua Kikuu (TB) kikamilifu kabla ya kuanza masomo.

Mhe. Ummy ametoa agizo hilo mapema leo katika ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO, mjini Dodoma alipokuwa akitoa tamko la Maadhimisho ya siku ya Kifua Kikuu Duniani yanayatarajiwa kufanyika  Machi 24 mwaka huu.

Mwaka  2017 tulikamisha tathmini ya awali ya hali ya TB mashuleni na kubaini kuwa kuna idadi kubwa ya Wanafunzi wanaougua TB na Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI  na Wizara Elimu tulitoa maagizo kwa Makatibu Tawala wa Mikoa kuhakikisha Wanafunzi wote hasa wa Bweni wanachunguzwa TB kabla ya kuanza shule,” alisema Mhe. Ummy.

Aidha, amesema kuwa  ni marufuku  kwa Madaktari kujaza fomu za uchunguzi wa Afya bila kumpima mwanafunzi husika, kufanya hivyo ni  kosa la jinai  hali inayoweza kuliangamiza Taifa kwa makusudi kwa uzembe ambao hauwezi kuendelea kuvumiliwa.

Mhe. Ummy amesema amekabidhi mashine tano za “gene- Xpert” kwa hospitali binafsi za Jijini Dar es Salaam ili kudhihirisha nia ya Serikali ya kutaka kila mtoa huduma kushiriki kikamilifu na kumfikia kila Mtanzania mwenye uhitaji wa matibabu ya TB.

Amezitaja hospitali hizo kuwa ni Aga khan, Kairuki, Regency Medical Center, TMJ na Hindul Mandal.  Mashine hizo zilizotolewa kila moja ina thamani ya Shilingi Milioni 38.

“Kwa kuanza tumeanza na hospitali hizi zenye kiwango kikubwa cha wagonjwa waohudumiwa na pia kwa kuzingatia utayari wa hospitali hizi katika kutoa huduma za TB sanjari na malengo ya Serikali yatu ya Awamu ya Tano katika kuhakikisha huduma za Afya zinawafikia Wananchi wake wote,” alisema Mhe. Ummy.

Kwa upande wake Mkurugenzi Huduma za Kinga Wizara ya Afya Maendeleo Jamii Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Leonard Subi amesema Serikali inashirikiana na Waganga wa Tiba asilia kwa kuwapa elimu ya dalili za Kifua Kikuu ili  waweze kuwasiliana na Waganga Wafawidhi mara tu wanapoona dalili hizo kwa wagonjwa.

Dkt. Subi amesema Waganga wa tiba asili wanasajiliwa kisheria na wapo katika maeneo ya mijini na vijijini.  Aidha amesema,  Serikali haiwatambui waganga wa jadi wanaopiga ramli.

Kifua Kikuu (TB) ni ugonjwa wa kuambukizwa kwa njia ya hewa na unaongoza kwa kusababisha vifo vingi Duniani. Kwa mujibu wa Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 10.4 huugua Kifua Kifuu kila mwaka Duniani na Milioni Moja kati ya hao ni watoto wenye umri chin i ya miaka 15.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *