Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Wafanyabiashara Tanga Wapewa Elimu ya Msamaha wa Kodi

Na Veronica Kazimoto – Tanga

Wafanyabiashara wapatao 150 mkoani Tanga wameelimishwa kuhusu Msamaha wa Riba na Adhabu ya Malimbikizo ya Madeni ya Kodi, Mabadiliko ya Sheria za Kodi ya Mwaka 2018 na Mfumo wa Maadili wa Watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa lengo la kuwawezesha wafanyabiashara hao kujua kwa undani masuala yanayohusu kodi pamoja na kuwahi kuomba msamaha wa riba na adhabu ambapo mwisho wa kutuma maombi ni tarehe 30 Novemba, 2018.

Akifungua semina ya wafanyabiashara hao mkoani hapa iliyoandaliwa na TRA, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Monica Kinara amesema kuwa, elimu hiyo imekuja wakati muafaka na siyo tu itawasaidia kujua masuala ya kodi bali wale wenye malimbikizo ya madeni ya kodi watanufaika na msamaha huo na hatimaye wataweza kulipa kodi kwa wakati.

“Ninawashukuru sana TRA kwa kuleta elimu hii hapa mkoani kwetu na ni matumaini yangu kuwa, wafanyabiashara mtatumia fursa hii vizuri ili iwasaidie kuelewa masuala mbalimbali yanayohusu kodi na hasa msamaha wa riba na adhabu ya kodi ili muweze kuomba msamaha huo ndani ya muda uliopangwa,” alisema Kinara.

Naye, Meneja wa Elimu kwa Mlipakodi kutoka TRA Makao Makuu Diana Masalla amewaeleza wafanyabiashara hao kwamba, ni jukumu la kila mwenye malimbikizo ya madeni ya kodi kuwahi kuomba msamaha wa riba na adhabu akiwa ameambatisha dodoso maalum la msamaha huo pamoja na ritani ya taarifa za Mlipakodi.

“Huu ni msamaha maalumu hivyo ni muhimu mzingatie kutuma maombi kabla ya tarehe 30 Novemba mwaka huu, kinyume na hapa mtaikosa fursa hii muhimu ambayo ina lengo la kuwapunguzia mzigo wa kodi,” alisisitiza Masalla.

Kwa upande wake Mfanyabiashara wa Nyumba za Kulala Wageni Teti Mathias ameshukuru ujio wa elimu hii mkoani Tanga na kuiomba TRA iwe na utamaduni wa kutoa elimu hizi katika ngazi ya Kata na Tarafa ili wafanyabiashara wengi waweze kupata uelewa wa kutosha kuhusu masuala mbalimbali ya kodi.

Msamaha maalum wa Riba na Adhabu kwenye Malimbikizo ya Madeni ya kodi unatolewa kwa asilimia 100 kwa wafanyabiashara wenye malimbikizo hayo ambao watakidhi vigezo vilivyowekwa katika utaratibu wa kuomba msamaha huo.

 

41 thoughts on “Wafanyabiashara Tanga Wapewa Elimu ya Msamaha wa Kodi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *