Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Wadau Waombwa Kujitokeza Kusaidia Maandalizi ya Mashindano ya Soka kwa Wenye Ulemavu Afrika Mashariki

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)kuhusu mashindano ya Shirikisho la mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu Afrika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Juni mwaka na kushirikisha nchi 5 wanachama.

Na : Mwandishi Wetu

Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu imewataka wapenzi na wadau wa soka nchini kushiriki  maandalizi ya mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu kwa watu wenye ulemavu Afrika Mashariki (CECAAF) yanayotarajiwa kufanyika nchini Mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.

Akizungumza  na waandishi wa habari  leo Mei 16, 2019 Jijini Dodoma,katika mkutano uliolenga kuitambulisha kamati ya wabunge watano waliojitolea kuhamasisha Watanzania,kushiriki kwa hali na mali katika mashindano hayo,  Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe, amesema kuwa mashindano hayo yatashirikisha nchi za Tanzania Bara, Zanzibar, Uganda, Kenya na Rwanda.

“Mashindano haya yatakayokuwa ya kwanza kufanyika katika ukanda huu wa Afrika yameanzishwa kwa mujibu wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa haki za Walemavu wa mwaka 2006, unaotaka haki ya Walemavu kushiriki katika mambo kadhaa ikiwemo michezo”

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati waliokaa) pamoja na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye ulemavu Mhe. Stella Ikupa (wa pili kutoka kushoto waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wabungu wa kamati iliyojitolea kuhamasisha ushiriki wa Watanzania katika mashindano hayo, mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo.

Akifafanua zaidi, Dkt. Mwakyembe amesema kuwa lengo la kuhamasisha umma wa watanzania ni kuunga mkono mashindano hayo kwa hali na mali.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi  ya Waziri mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu Mhe. Stella Ikupa amesema kuwa mashindano hayo yatasaidia kuibua vipaji vya watu wenye ulemavu na hivyo kushiriki katika kukuza sekta ya michezo.

Pia ameiomba jamii kwa upana kujitokeza kuchangia na kushiriki mashindano hayo kwa kuzingatia kuwa watu wenye ulemavu wana nia ya kushiriki vyema katika mashindano hayo.

Naye mbunge wa Sengerema mhe. William Ngeleja,ambaye pia ni mwenyekiti wa klabu ya michezo ya Bunge, akizungumza kwa niaba ya Spika wa Bunge, amesema  kuwa watashiriki kikamilifu katika kuhakikisha kuwa mashindano hayo yanafanikiwa kwa kuzingatia malengo yake.

Mheshimiwa Ngeleja,aliongeza kusema kuwa watashiriki kwa vitendo kwa kuzingatia  kuwa Bunge ni wasimamizi  wa  sheria za sekta ya michezo ,mikataba ya kimataifa, sheria na kanuni  katika sekta hii.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri mkuu Wenye Ulemavu mhe. Stella Ikupa akisisitiza jambo wakati wa mkutano wa waandishi wa habari kuhusu mashindano ya Shirikisho la mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu Afrika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Juni mwaka na kushirikisha nchi 5 wanachama wakati wa mkutano huo.

Wizara ya Habari kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, inawaomba wananchi kuipa Kamati hii ya wabunge ushirikiano wakutosha katika maandalizi ya michuano hiyo ambayo inahitaji fedha ya kutosha na vifaa.

Wabunge wanaounda kamati hiyo ni Mheshimiwa William Ngeleja,Mheshimiwa Venance Mwamoto,Mheshimiwa Margareth Sitta, Mheshimiwa Amina Mollel na Mheshimiwa Riziki Said Lulida.

Mbunge wa Sengerema mhe. William Ngeleja,ambaye pia ni mwenyekiti wa klabu ya michezo ya Bunge akichangia jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari ili kuhamasisha jamii kushiriki katika mashindano ya Shirikisho la mpira wa miguu kwa watu wenye ulemavu Afrika Mashariki yanayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Juni mwaka na kushirikisha nchi 5 wanachama.

(Picha na PMO)

3 thoughts on “Wadau Waombwa Kujitokeza Kusaidia Maandalizi ya Mashindano ya Soka kwa Wenye Ulemavu Afrika Mashariki

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama