Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Wadau wa Maendeleo Kuchagia Bilioni 98.1 Kupitia Mfuko wa Afya wa Pamoja

Waziri Ummy amesema katika mwaka wa fedha uliopita, wadau kupitia Mfuko walichangia kiasi cha Shilingi bilioni 74.3 ambapo asilimia 90 ya fedha zimekwenda kwenye Halmashauri na zimeingizwa moja kwa moja kwenye Zahanati, Vituo vya Afya pamoja na Hospitali za Wilaya nchini.

Aidha, Waziri Ummy Mwalimu amesema upo umuhimu kwa wadau wa maendeleo kuchanga fedha kwa pamoja na kuweka kwenye Mfuko wa Afya wa pamoja na kusema kuwa kufanya hivyo ni kuzingatia mifumo na taratibu za Serikali za kutoa fedha kwa ajili ya Huduma za Afya nchini pamoja na kuwekeza fedha kwenye maeneo ya vipaumbele vya Serikali.

“Fedha zinazoingizwa nchini kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali za afya tunapenda ziingizwe kwenye Mfuko wa Afya wa pamoja ili tuweze kushirikiana kufanya kazi pamoja na kupata matokea ya haraka kwa pamoja. Mapendekezo yetu wadau wengine wachangie kupitia mfuko huo kwani tumeona mafanikio makubwa”, amefafanua Waziri Ummy Mwalimu.

Kwa upande wake Naibu Waziri kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Dkt. Festo Dugange ameshukuru wadau hao kwa kuendela kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Mhe. Dugange amepongeza wadau hao kwa kuongeza kiwango cha fedha kutoka Shilingi bilioni 74.3 mwaka wa fedha 2021/22 hadi bilioni 98.1 kwa mwaka wa fedha 2022/23 na kusema kuwa kupitia mchango huo pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanyika, Serikali kufanya mapinduzi makubwa kwenye ubora wa huduma za afya kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

Mhe. Dkt. Dugange amesema kuwa asilimia 33.3 ya fedha hizo hutumika kwenda kununua dawa, vifaa tiba na ‘reagents’ kwa ajili ya vipimo vya maabara ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za mama na mtoto katika vituo vya kutolea huduma za afya.

“Kwa mwaka huu wa fedha 2022/23, vituo zaidi ya 175 vimepata vifaa tiba kwa ajili ya huduma za upasuaji lakini kwa mwaka ujao wa fedha, tunatarajia vituo zaidi ya 225 vitapata vifaa tiba”, amefafanua Mhe. Dugange.

Akizungumza kwa niaba ya Wadau wanaochangia katika Mfuko wa Afya wa pamoja, akizungumza na Vyombo vya Habari, Dkt. Peter Nyela Meneja wa Program ya Afya kutoka Ubalozi wa ‘Ireland’ wanafanya hivyo kusaidia Serikali ili kuhakikisha Vituo vya kutolea huduma za afya nchini vinakuwa na dawa, kurahisisha huduma nyinginezo ikiwemo huduma za rufaa, pamoja na motisha kwa watoa huduma za afya nchini.

Huu ni ushirikiano mzuri sana baina ya Serikali na Wadau wa Maendeleo kuweza kufanya kazi kwa pamoja kuweza kusaidia kuboresha huduma za Afya nchini, Sisi kama Wadau kwa pamoja tutaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuboresha Sekta ya Afya nchini”, amefafanua Dkt. Nyela.

Mfuko wa Afya wa Pamoja umedumu kwa miaka 23 hadi kufikia leo ambapo ni muunganiko wa pamoja baina ya Serikali na Wadau wa Maendeleo kutoka Denmark, Korea, Ireland, Switzerland, Canada, UNFPA, UNCEF na Benki ya Dunia ambao huchangia katika huduma za afya nchini kwa kutoa fedha na kuziweka kwenye akaunti moja na fedha hizo kutolewa moja kwa moja kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

8 thoughts on “Wadau wa Maendeleo Kuchagia Bilioni 98.1 Kupitia Mfuko wa Afya wa Pamoja

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama