Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Wachimbaji Wadogo Handeni Kunufaika na Kituo cha Umahiri

Mkuu wa Wilaya ya Handeni Bw. Godwin Gondwe akisisitiza umuhimu  wa Kituo cha umahiri  kwa wachimbaji wadogo wa madini Wilayani Handeni kinachojengwa na Wizara ya Madini ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuinua wachimbaji hao katika Wilaya hiyo na maeneo yote ya mikoa ya jirani na Wilaya hiyo.

Serikali Wilayani Handeni imewataka wananchi kutumia fursa ya kujengwa kwa Kituo cha umahiri katika Wilaya hiyo kujiletea  maendeleo kupitia sekta ya madini.

Akizungumza katika mahojiano maalum kuhusu ujenzi wa kituo hicho kinachojengwa na Wizara ya Madini kupitia mkandarasi ambaye ni SUMA JKT,  Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Godwin Gondwe amesema hiyo ni fursa  adhimu kwa wananchi wa Wilaya hiyo kwa kuwa watajengewa uwezo wa namna bora ya kushiriki katika uchimbaji wa madini kwa kuzingatia sheria na kanuni zinazosimamia sekta hiyo.

“Wananchi sasa hawatahitaji kusafiri kwenda mikoa mingine kujifunza namna ya kuchimba madini, kuchenjua na hata kushiriki katika kuendeleza sekta hii kwa kuwa kituo cha umahiri  ( Centre of  Excellence) kinajengwa hapa Handeni hivyo ni jambo la kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuona kuwa kuna umuhimu wa kuwainua wachimbaji wadogo kwa kuwaongezea ujuzi” Alisisitiza Mhe. Gondwe.

Luteni  Khalfani Mturi  kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT)akipokea ramani ya Kituo cha umahiri (Centre of Excellence) kwa wachimbaji wadogo wa madini kwa niaba ya Meneja wa ujenzi wa SUMA JKT Kanda ya Kaskazini Meja. Daudi Zengo  kutoka kwa Mshauri muelekezi wa mradi huo Bw. Beno Matata kutoka Kampuni ya Inter Consult Ltd, mradi huo unatekelezwa na Wizara ya Madini katika Wilaya ya Handeni, kupitia Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini unaotekelezwa na Wizara ya Madini  ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Serikali katika kuwainua wachimbaji wadogo.

Akifafanua Gondwe amesema kuwa Wilaya hiyo ina hazina kubwa ya madini ya aina mbalimbali ambayo hayajachimbwa hivyo ujenzi wa kituo hicho utasaidia katika kuimarisha usimamizi wa rasilimali hizo na kuwainua wananchi kwa kuwa watachimba madini hayo kwa kuzingatia sheria ikiwemo kulipa kodi zote na hivyo kuondoa tatizo la uwepo wa wachimbaji wasiozingatia weledi na sheria ya madini.

Kwa upande wake mwakilishi wa SUMA JKT. Luteni Khalfani Mturi akizungumza kwa niaba ya Meneja wa ujenzi Kanda ya Kaskazini Meja Daudi Zengo  amesema kuwa dhamira yao baada ya kukabidhiwa eneo la ujenzi wa mradi ni kuhakikisha kuwa mradi unakamilika kwa muda uliopangwa kwa kuzingatia ubora na mkataba wa mradi huo kati yao na Wizara ya Madini inayotekleza mradi huo.

Msanifu majengo wa Kampuni ya Inter Consult Ltd Bw. Beno Matata akieleza mikakati ya kampuni hiyo katika kuhakikisha kuwa inasimamia mradi huo wa ujenzi wa Kituo cha Umahiri kitakachowanufaisha wachimbaji wadogo kinachojengwa Wilayani Handeni ikiwa ni sehemu ya Juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Madini kuinua wachimbajin hao.

Aliongeza kuwa jukumu kubwa sasa ni kuanza utekelezaji wa ujenzi wa kituo hicho ili kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.

Kwa upande wake Mjiolojia kutoka Wizara ya Madini Bi. Veronica Nangale amesema kuwa wanamatumaini kuwa mkandarasi ambaye ni SUMA  JKT atakamilisha mradi  kwa wakati na kwa kuzingatia mkataba wa mradi huo.

Mjiolojia wa Wizara ya Madini Bi. Veronica Nangale akisisisitiza jambo  kwa mkuu wa Wilaya ya Handeni Bw. Godwin Gondwe (hayupo pichani) wakati walipomtembelea Ofisini kwake kabla ya hafla ya kukabidhiwa kwa eneo kitakapojengwa kituo  cha umahiri(Centre of Excellence) kwa wachimbaji wadogo wa madini, hafla hiyo ilifanyika Wilayani Handeni, ujenzi wa kituo hicho unafanyika kupitia  Mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini unaotekelezwa na Wizara ya Madini  ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Serikali katika kuwainua wachimbaji wadogo

Naye Msanifu Majengo kutoka kampuni ya InterConsult  Ltd inayosimamia mradi huo Bw. Beno Matata amesema kuwa Kampuni hiyo itasimamia mradi huo kwa kuzingatia  weledi ili ukamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa kwa mujibu wa mkataba na sheria za ujenzi.

Kujengwa kwa kituo cha umahiri katika Wilaya ya Handeni kutasaidia wachimbaji wadogo kujengewa uwezo wa kuchenjua madini kwa kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira, biashara ya madini, mafunzo ya usalama na afya sehemu za kazi, utunzaji wa mazingira kwenye migodi.

Luteni  Khalfani Mturi  kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) akisisitiza jambo mara baada ya kukabidhiwa eneo na ramani ya Kituo cha Umahiri kwa wachimbaji wadogo wa madini kinachojengwa na mkandarasi SUMA JKT, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Wizara ya Madini kuimarisha sekta hiyo na kuwainua wachimbaji wadogo.

Ujenzi wa vituo vya umahiri unatekelezwa kupitia mradi wa Usimamizi Endelevu wa Rasilimali Madini “Sustainable Management of Mineral Resouces Project- SMMRP”, Vituo hivyo vinajengwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini ambapo mradi huo unathamani ya jumla ya zaidi ya bilioni 11 zitakazotumika kujenga vituo hivyo katika maeneo mbalimbali ikiwemo Handeni Mkoani Tanga.

Afisa Mipango mji wa Wilaya ya Handeni Bw. Byabato William akisisitiza jambo kwa Luteni  Khalfani Mturi  kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wakati  wan halfa ya kukagua na kukabidhi eneo litakalotumika kujenga kituo cha Umahiri kinacholenga kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo Wilayani Handeni.

Msanifu majengo wa Kampuni ya Inter- Consult Ltd Bw. Beno Matata akisisitiza jambo wakati akikabidhi ramani za Kituo cha Umahiri kwa Lt. Luteni  Khalfani Mturi  kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambapo kituo hicho kitajengwa na SUMA JKT ikiwa ni juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Madini Kuwainua wachimbaji wadogo.

(Picha zote na Frank  Mvungi- MAELEZO, Handeni- Tanga)

32 thoughts on “Wachimbaji Wadogo Handeni Kunufaika na Kituo cha Umahiri

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *