Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Wachimbaji Geita Watakiwa Kuzingatia Matumizi Salama ya Kemikali

 

Mgeni Rasmi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Esther Hellen Jason (aliyesimama) akiongea wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa wachimbaji na wachenjuaji wa madini ya dhahabu katika Mkoa wa Geita yaliyoanza leo katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Geita. Kushoto ni Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko na wengine kutoka kulia ni Meneja wa Maabara ya Kanda ya Ziwa, Bonaventura Masambu (wa pili kulia) na Meneja wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Ziwa, Mhandisi Redempta Samwel.

Na; Mwandishi wetu- Geita

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Esther Hellen Jason amewataka wachimbaji na wachenjuaji wa dhahabu katika Mkoa wa Geita kuzingatia matumizi salama ya kemikali wakati wa uchimbaji wa dhahabu ili kulinda afya zao na mazingira.

Mwenyekiti wa Bodi ameyasema hayo leo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa wadau hao wa kemikali yaliyoanza leo katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Geita na kuandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Kanda ya Ziwa.

“Mkoa wa Geita una wachenjuaji wa madini aina ya dhahabu kwa njia ya Vat leaching 326 na Elution 36. Pia inao wachenjuaji wa kutumia kemikali ya zebaki 3076. Wachenjuaji hawa wote wanatumia kemikali mbalimbali kuanzia aina moja hadi kumi na tano, zikiwemo Zebaki na Cyanide. Watumiaji wa kemikali hizi wengi wao wana uelewa mdogo au hawana uelewa kabisa wa Sheria inayosimamia na kudhibiti matumizi yasiyo salama ya kemikali”Alissitiza Prof. Jason

Profesa Jason, aliwataka washiriki wa mafunzo kutumia elimu watakayoipata kujikinga na madhara ya kemikali na kuipeleka elimu hiyo kwa wachimbaji wenzao ambao hawajafanikiwa kuhudhuria ili kuwasaidia kujikinga katika kazi za uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu.

Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko (wa pili kushoto), akiongea kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Profesa Esther Hellen Jason (aliyekaa katikati) kufungua mafunzo kwa wachimbaji na wachenjuaji wa dhahabu mkoani Geita.

“Wafikishieni elimu hii wenzenu ambao hawajaweza kuhudhuria mafunzo haya  maana wengine ni marafiki, wazazi na watoto wenu, hivyo mnao wajibu wa kuwalinda kwa kuwapatia elimu hii mtakayoipata kupitia mafunzo haya ili kuwasaidia kulinda afya na mazingira kutokana na madhara ya kemikali na kuepusha kupata maradhi kama ya saratani,upofu na mfumo wa upumuaji na fahamu”alimaliza.

Akiongea kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, alisema washiriki watafundishwa taratibu za utumiaji kemikali kulingana na matakwa ya Sheria na Kanuni ili zisilete madhara kwa jamii na mazingira. Pia, alieleza kuwa watajifunza madhara mbalimbali yanayoweza kusababishwa na kemikali, namna ya kujikinga, kukinga wengine na kuzuia uharibifu wa mazingira.

“Mafunzo yameletwa kwenu na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Kanda ya Ziwa kwa lengo la kuwajengea uelewa juu ya matumizi ya kemikali mbalilmbali na madhara yatokanayo na kukiuka Sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha mnakuwa na matumizi sahihi na salama ya kemikali katika shughuli zenu ili kulinda afya na mazingira mnayofanyia kazi.”

Aidha, Katibu Mkuu wa Chama cha Wachimbaji madini Mkoa wa Geita, Golden Hainga, aliwasisitiza washiriki kusikiliza kwa umakini mafunzo na kutumia elimu hiyo katika uboreshaji wa shughuli za uchimbaji kwenye maeneo yao.

“Tutumie fursa hii ya mafunzo kubadilika katika uchimbaji wetu na kuongeza uzalishaji wa dhahabu kulingana na matumizi sahihi ya kemikali.”

 

Mgeni Rasmi, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Esther Hellen Jason akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo kwa wachimbaji na wachenjuaji wa madini ya dhahabu katika Mkoa wa Geita yaliyoanza leo katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Geita. Kushoto ni Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko na wengine kutoka kulia ni Meneja wa Maabara ya Kanda ya Ziwa, Bonaventura Masambu (wa pili kulia) na Meneja wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Ziwa, Mhandisi Redempta Samwel.

Meneja wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Ziwa, Mhandisi Redempta Samwel akizungumza wakati wa mafunzo kwa wachimbaji na wachenjuaji wa madini ya dhahabu katika Mkoa wa Geita yaliyoanza leo katika Ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Geita.

327 thoughts on “Wachimbaji Geita Watakiwa Kuzingatia Matumizi Salama ya Kemikali

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama