Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Vijana nchini wameaswa kuanzisha miradi ya kimkakati ili kujiletea maendeleo

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (Mb) akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Iringa mara baada ya kuwasili ofisini hapo kwa ajili ya ziara ya kuhamasisha vijana na kukagua maeneo yaliyotengwa kujenga vitalu nyumba mkoani humo.

Na; mwandishi wetu:

Vijana nchini watakiwa kubadili mtazamo kwa kuanzisha miradi ya kimkakati itakayowawezesha kiuchumi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (Mb) alipofanya ziara hiyo Mkoa wa Iringa kwa lengo la Kuhamasisha na kukagua maeneo ya ujenzi wa Vitalu Nyumba (Green House) na uwepo wa miundombinu itakayotumika kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Mhagama amesema sekta ya kilimo inaajiri na kuchangia katika pato la taifa kwa zaidi ya asilimia 60%, hivyo vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa wakatumie rasilimali ardhi kama mtaji wa kujiajiri na kuweza kuajiri wenzao.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Richard Kasesela akieleza jambo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipofanya ziara mkoani humo ya kukagua maeneo ya kujenga vitalu nyumba. (Wa kwanza kushoto) ni Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Bw. Fikira Kisimba.

“Lengo letu ni vijana kutumia sekta hii ya umahiri kwa ajili ya kuwaondoa kwenye mitazamo finyu na kuwa na mitazamo chanya ili waweze kunufaika na miradi itakayo buniwa na kutumika kama mfano kwa vijana nchi nzima.” Alisema Waziri Mhagama

Aliongeza kuwa vijana watafundishwa kilimo cha Kitalu nyumba ambavyo vitawawezesha kuongeza thamani kwenye mazao watakayozalisha na mradi huo ukawe sehemu ya ajira zao.

Aidha, Waziri Mhagama alitoa rai kwa vijana kuwa chachu ya maendeleo ya uchumi wa taifa kwa kushirikiana kwa pamoja bila kujali itikadi zao ili kutimiza adhma ya vijana wote.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iringa alisela mradi huo utawawezesha vijana wa mkoa wa iranga kuweza kuondokana na changamoto ya ajira kwa kuwa Serikali imewaletea teknolojia hiyo itakayo wawezesha vijana kujiajiri.

Baadhi ya Maafisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu waliombatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama katika ziara ya kukagua maeneo ya kujenga vitalu nyumba. (Kulia ni) Afisa Vijana Mwandamizi Bw. Gedfrey Massawe na Afisa Kazi Bi. Neema Moshi. (Kushoto ni) Afisa Elimu wa Mkoa Bw. Richard Mfugale.

Naye mmoja wa vijana aliweza kuishukuru Serikali kwa kuanzisha mradi huo wenye tija ya kuwanufaisha vijana wote katika kuwaletea mabadiliko na ukombozi wa kiuchumi.

“Mradi huu utatuwezesha sisi vijana kunufaika na teknolojia hii ya kilimo cha kisasa kwa kuanzisha miradi itakayotusaidia kujipatia mtaji.”

Katika Ziara hiyo Waziri Mhagama alitembelea Chuo cha Ihemi kwa ajili ya kukagua majengo yatakayokuwa yanatumia kufundishia vijana elimu ya ujasiriamali na kilimo cha kitalu nyumba (Green House).

(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


FacebooktwittermailFacebooktwittermail