Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Uzalishaji wa Mazao ya Chakula Waimarika Nchini

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuahirisha Mkutano wa 12 wa Bunge jijini Dodoma, Septemba 14, 2018.

Na Jacquiline Mrisho – Dodoma

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amesema kuwa hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula na upatikanaji wake nchini umeendelea kuimarika.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo mjini Dodoma alipokuwa akitoa hoja ya kuahirisha Mkutano wa 12 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutangaza kuanza kwa mkutano ujao mnamo Novemba 6 mwaka huu.

Mhe. Majaliwa amefafanua kuwa tathmini iliyofanyika mnamo mwezi Juni, 2018 imeonyesha kwamba uzalishaji wa mazao ya chakula katika msimu wa mwaka 2017/18 ni tani milioni 16.9 ambapo kati ya hizo tani milioni 9.5 ni mazao ya nafaka na tani milioni 7.4 ni mazao yasiyo ya nafaka.

“Kutokana na uzalishaji huo na kwa kuzingatia mahitaji ya chakula nchini ambayo ni tani milioni 13.6, kutakuwa na ziada ya tani milioni 3.3 hivyo nchi itajitosheleza kwa chakula kwa asilimia 124,”alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Mhe. Majaliwa ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuwasihi wananchi kutumia akiba hiyo ya chakula kwa uangalifu kwani zipo nchi jirani ambazo zina uhaba mkubwa.

Vile vile ameziagiza taasisi zote zinazosimamia elimu ya lishe na afya kuongeza nguvu zaidi katika kutafuta mbinu bora na kutoa elimu kwa wananchi ili kupunguza kiwango udumavu na utapiamlo hususan kwa watoto wadogo.

Akizungumza kuhusu upatikanaji wa pembejeo za kilimo nchini, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali inaendelea kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa pembejeo muhimu za kilimo kwa wakati ambapo katika msimu wa kilimo wa mwaka 2018/19 upatikanaji wa mbolea aina zote umefikia kiasi cha tani 215,207 wakati matarajio ya matumizi ya mbolea hiyo ni tani 485,000.

Aidha, Serikali itahakikisha upatikanaji na matumizi sahihi ya viuatilifu kwa mazao mbalimbali na kwamba kwa msimu wa mwaka 2018/19 Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 10  kwa ajili ya kupambana na wanyama pamoja na wadudu waharibifu.

 


FacebooktwittermailFacebooktwittermail