Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Uwepo wa Chumba cha Watoto Wenye Matatizo ya Moyo JKCI Waharakisha Matibabu Yao

Picha ya Jengo jipya la watoto la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) ambalo lina ofisi nane, vyumba vya madaktari vinne, wodi yenye vitanda 41 kati ya hivyo 23 viko katika wodi ya kawaida, nane chumba cha uangalizi maalum (ICU) na 10 wodi ya kulipia. Kuwepo kwa jengo hilo kutaboresha huduma za matibabu ya moyo kwa watoto.

Na Mwandishi  maalum

Kuwepo kwa chumba cha watoto wenye matatizo ya moyo walioko katika uangalizi maalum (ICU) katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kumesaidia kwa kiasi kikubwa kuharakisha utolewaji wa matibabu yao.

Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Idara ya watoto wenye magonjwa ya moyo Dkt. Sulende Kubhoja wakati akiongea na mwandishi wa habari hizi.

Dkt. Kubhoja alisema chumba hicho chenye vitanda nane kipo katika wodi mpya ya watoto ambayo imejengwa na kufanyiwa ukarabati imeanza  kutumika mwanzoni mwa wiki hii.

“Mwanzo ilikuwa ni changamoto pale ambapo mtoto alitakiwa kupata huduma ya dharula na kulazwa katika chumba cha uangalizi maalum lakini kuwepo kwa ICU yao kutaharakisha upatikanaji wa huduma hiyo”.

Wazazi wakiwa katika jengo jipya la watoto la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kuwapeleka watoto wao kwa madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kupata matibabu.

“Kabla ya kuanza kutumika kwa jengo hili watoto walikuwa wanatibiwa katika jengo ambalo watu wazima walikuwa wanatibiwa na hivyo kutokuwa na nafasi ya kutosha. Hivi sasa watoto wana jengo lao ambalo lina nafasi kubwa na kuwafanya wapate nafasi ya kucheza tofauti na ilivyokuwa awali”, alisema Dkt. Kubhoja.

Alisema kutokuwachanganya watoto na watu wazima kutaboresha huduma kwani dawa na vifaa tiba zitakuwa kwa ajili ya watoto na mazingira ya cliniki na wodini yatakuwa rafiki kwao tofauti na ilivyokuwa awali.

Kwa upande wake Afisa Muuguzi ambaye ni  msimamizi wa wodi ya watoto Husna Mzungu alisema kukamilka kwa ukarabati wa jengo hilo ni jambo jema na la furaha kwani kumebadilisha muonekano wa wodi ya watoto ukilinganisha na ilivyokuwa awali.

Husna alisema katika jengo hilo jipya kuna vitanda vya kutosha ambavyo vinasaidia kuwaweka watoto katika mazingira ya nafasi na kuweza kulala mmoja mmoja ukilinganiha na wodi  ya zamani  ambako kulikuwa na vitanda vichache  vya watoto, hivyo kukiwa na wagonjwa wengi walikuwa wanapata tabu.

Jengo hilo  lina ofisi nane, vyumba vya madaktari vinne, wodi yenye  vitanda 41 kati ya hivyo  23 viko katika wodi ya kawaida, nane chumba cha uangalizi maalum (ICU)  na  10 wodi ya  kulipia.

Gharama za ujenzi na ukarabati wa jengo hilo ni shilling bilioni 1.3 ambapo asilimia 60 ya fedha hizo zimetolewa  na Serikali na asilimia 40 zimetolewa na Jumuia ya Kihundu nchini (BAPS Charity).

 

One thought on “Uwepo wa Chumba cha Watoto Wenye Matatizo ya Moyo JKCI Waharakisha Matibabu Yao

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *