Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Utapiamlo ni Kikwazo cha Ukuaji wa Uchumi-Majaliwa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema utapiamlo ni miongoni mwa vikwazo vya  kutimiza dhamira ya Serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa viwanda ambao utawezesha Taifa kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. 

 Amesema bila ya kuwa na lishe bora na afya njema, vinavyosaidia kuongeza uwezo wa kuelewa na ubunifu ili kuhimili ushindani wa kiuchumi nchi haitafika kwa wakati kwenye uchumi wa kati na wa viwanda uliokusudiwa.

 Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Oktoba 3, 2019) wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Wadau wa Lishe uliofanyika kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma. Amesema ni muhimu elimu ya lishe ikatolewa kwa wananchi wote.

 “Pamoja na tafiti kuonesha kwamba tumepunguza viwango vya udumavu na upungufu wa damu bado viwango vyake havikubaliki kimataifa. Vilevile, tuna viwango vya utapiamlo ambavyo vimezidi kuongezeka na havikubaliki kimataifa ikiwemo uzito uliozidi kwa wanawake wenye umri wa kuzaa.”

 Amesema hali hiyo ni hatari kwa nchi ambayo inayokabiliwa na aina nyingine za utapiamlo unaosababishwa na lishe duni kama udumavu, utapiamlo mkali na wa kadiri ambapo athari zake ni kubwa katika ukuaji wa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano. “Hii ni ishara tosha kwamba tunatakiwa kuongeza juhudi katika kupambana na aina zote za utapiamlo ili kufikia viwango vinavyokubalika Kimataifa.”

 Amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau itaendelea kutoa kipaumbele kwa maeneo ambayo yameathirika zaidi na ambayo yanatekeleza  miradi inayolenga kupunguza udumavu kwa watoto, matatizo ya upungufu wa vitamin na madini.

 Kipaumbele kitatolewa katika kuimarisha matibabu ya utapiamlo mkali na wa kadiri, kupunguza tatizo la uzito uliokithiri na viriba tumbo na tatizo la upungufu wa damu kwa wanawake na watoto ili kuhakikisha kuwa miradi hiyo inaleta matokeo chanya katika maeneo hayo.

 Amesema kuwa mipango yoyote wanayojiwekea haiwezi kuleta matokeo chanya bila kuitengenezea mikakati thabiti ya utekelezaji ikiwa ni pamoja na kutenga rasilimali za kutosha, ambapo wataalamu hao waibue mikakati itakayoweza kutumika katika kupunguza tatizo la utapiamlo.

 Pia, Waziri Mkuu amewataka waajiri wote waandae fursa na kuwaalika mahala pa kazi maafisa lishe ili kuongeza ufahamu wa watumishi kuhusu lishe bora. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais-TAMISEMI zimetakiwa ziweke mipango ya kuhakikisha maafisa lishe wanaalikwa kutoa elimu sambamba na ufundishaji shuleni.

 Kwa upande wake,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Jenista Mhagama amesema bila kuwa na nguvu kazi yenye lishe na afya bora Taifa haliwezi kufanikiwa kwenye masuala ya elimu, kilimo, viwanda hivyo kukwamisha jitihada za Serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa viwanda.

“Kwa hali iliyopo sasa ni wazi kuwa bado tuna kazi kubwa ya kufanya ili kuondokana na utapiamlo nchini. Juhudi za pamoja zinahitajika ili kuweza kufikia malengo tuliyojiwekea katika Mpango Jumuishi wa Taifa wa Lishe (2016/17 – 2020/21), ambayo ni pamoja na kupunguza udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kufikia asilimia 28 na uzito uliozidi kufikia asilimia 30.”

Amesema Serikali inatambua kuwa lishe ni suala mtambuka linalotegemea jitihada za sekta mbalimbali, ambapo waliandaa Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa miaka mitano kuanzia mwaka 2015/16 hadi 2020/21 ili kutoa muongozo katika utekelezaji wa afua mbalimbali za masuala ya lishe.

 Naye, Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda amesema katika jitihada za kupambana na umasikini ni vema elimu ya lishe bora ikatolewa kwa wananchi wote, ambapo amemshauri Waziri Mkuu aibebe agenda ya lishe, ambapo Waziri Mkuu amekubali.

 Waziri Mkuu huyo Mstaafu ameongeza kuwa, mila potofu nazo zimechangia suala la utapiamlo nchini kwa sababu katika familia nyingi nchini vyakula vingi vizuri wanapewa wanaume na vyakula vibovu wanakula wanawake na Watoto.

 Awali, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndungulile amesema udumavu umepungua kutoka asilimia 34.4 mwaka 2015 na kufikia asilimia 31.5 mwaka huu.

 Dkt. Ndungulile alisema licha kupungua kwa udumavu, changamoto iliyopo kwa sasa ni suala la unyonyeshaji kwa watoto walio na umri wa chini ya miezi sita, wanaonyenyeshwa ni asilimia 58 tu, huku asilimia 30 ya Watoto wenye umri wa zaidi ya miezi sita hawalishwi vizuri.”Theruthi moja ya wanawake nchini wana viribatumbo na utapiamlo wa lishe iliyopitiliza.

308 thoughts on “Utapiamlo ni Kikwazo cha Ukuaji wa Uchumi-Majaliwa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama