Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Ushiriki wa Wananchi Katika Miradi ya Kimkakati Kuchochea Ukuaji wa Uchumi

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (Mb) akizungumza na wadau kutoka kwenye Wizara, Idara na Taasisi za Serikali wakati wa ufunguzi wa warsha ya majadiliano na kupitia mwongozo wa kitaifa wa ushiriki wa wananchi katika uwekezaji hii leo Oktoba 16, 2018 Jijini Dodoma.

Frank Mvungi- MAELEZO, Dodoma

Serikali imewataka wananchi kutumia fursa ya uwekezaji mkubwa unaofanyika hapa nchini katika kujiletea maendeleo kupitia miradi hiyo ikiwemo ule wa ujenzi wa reli ya kisasa na ule wa kufua umeme Rufiji.

Akizungumza wakati akifungua warsha ya wadau yenye lengo la kupata maoni yatakayowezesha kukamilika kwa muongozo wa kitaifa katika kuwashirikisha wananchi kunufaika na fursa za miradi hiyo, Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu mhe. Jenista Mhagama  (Mb) leo Jijini Dodoma amesema kuwa Dhamira ya Serikali ni kuona watanzania wananufaika na fursa za kuwepo kwa miradi hiyo.

“ Katika mradi wa ujenzi wa daraja la juu pale Tazara jumla ya ajira zilizozalishwa ni 616 ambapo kati ya hizo 589 zilichukuliwa na watanzania na 27 raia wa kigeni na hii ni ishara nzuri kuwa sasa wananachi wameanza kunufaika na miradi hii, pia katika ununuzi wa huduma makampuni 15 yalishiriki ambapo ya watanzania ni 14 na 1 kutoka nje”; Alisisitiza  Mhagama.

Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Dkt. Festus Limbu akizungumza na wadau walioshiriki katika warsha ya majadiliano na kupitia mwongozo wa kitaifa wa ushiriki wa wananchi katika uwekezaji.

Akifafanua amesema kuwa Kila Wizara na Taasisi ya Serikali inatakiwa kuzingatia kuwa, ushiriki wa wananchi katika miradi inayotekelezwa unapewa kipaumbele kutokana na fursa zilizopo katika miradi husika ili kuhakikisha kwamba wananchi wanashiriki kikamilifu katika miradi ya kimkakati inayotekelezwa ikiwemo ule wa kufua umeme wa Rufiji, ujenzi wa viwanja vya ndege, mradi wa reli ya kisasa na ule wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Bandari ya Tanga.

Aliongeza kuwa lazima  Wizara na taasisi ziweke mfumo madhubuti wa ufuatiliaji ushiriki wa wananchi katika miradi yote inayotekelezwa, hali itakayowezesha kutoa taarifa pale inapohitajika, na kuwa na mipango inayoainisha masuala ya ajira kwa watanzania, manunuzi ya huduma, mpango wa kuongeza ujuzi kwa watanzania na pia kurithisha ujuzi ikiwa wataalamu watatoka nje ya nchi.

“ Serikali ya Awamu ya Tano inataka wananchi wamiliki uchumi ndio maana Baraza la Uwezeshaji wananchi kiuchumi tumelipa jukumu la kuhakikisha kuwa muongozo huo unakamilika kabla ya mwezi Desemba mwaka huu ili uanze kutumika kuwaletea wananchi maendeleo kupitia ushiriki wao katika miradi hii na fursa zitakazotokana nayo” ;Alisisitiza  Mhagama.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Bi. Beng’i Issa akielezea jambo kwa wadau juu ya mwongozo wa kitaifa wa ushiriki wa wananchi katika uwekezaji walipokutana Jijini Dodoma Oktoba 16, 2018.

Pia  Mhe. Mhagama aliwaasa watanzania kuhakikisha kuwa wanazingatia ubora wa huduma na bidhaa wanazotoa pale wanapopewa fursa yakufanya hivyo katika miradi inayotekelezwa ili kukuza soko na kupanua wigo wa huduma na bidhaa zao katika soko la ndani na nje.

Kwa upande wake Bw. Kadari Singo akizungumza kwa niaba ya Mtendaji mkuu wa Taasisi ya Uongozi amesema kuwa mjadala huo ni muhimu katika kipindi hiki ambapo taifa linalelekea katika ujenzi wa uchumi wa kati hali inayotoa fursa kwa wananchi na wamailiki wa Kampuni hapa nchini kutumia fursa zinazotokana na miradi inayoteklezwa kujiletea maendeleo kupitia huduma watakazoshiki kutoa katika miradi hiyo.

Aliongeza kuwa hakuna sababu ya watekelezaji wa miradi mikubwa inayotekelezwa kuagiza bidhaa zinazopatikana hapa nchini  wakati wananchi wanaweza kuzizalisha , bidhaa kama vyakula  vinaweza kuzalishwa hapa nchini alibainisha.

Baraza la Taifa la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi kwa kushirikiana na Taasisi ya Uongozi wameandaa warsha ya wadau ili kukamilisha mchakato wa kuzalishwa kwa muongozo wa Kitaifa utakaosaidia wananchi kushiriki kikamilifu katika miradi ya kimkakati inayotekelezwa hapa nchini.

Mkuu wa Idara ya Elimu kwa Viongozi kutoka Taasisi ya Uongozi, Bw. Kadari Singo akizungumza na wadau wakati wa mkutano huo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akijadili jambo na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Dkt. Festus Limbu wakati wa ufunguzi wa warsha ya majadiliano na kupitia mwongozo wa kitaifa wa ushiriki wa wananchi katika uwekezaji.

Wadau kutoka kwenye sekta mbalimbali wakisikiliza hotuba Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama alipokuwa akifungua warsha ya majadiliano na kupitia mwongozo wa kitaifa wa ushiriki wa wananchi katika uwekezaji iliyofanyika ukumbi wa LAPF, Jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akiwa katika picha ya pamoja na wadau walioshiriki baada ya kufungua warsha ya kujadili na kupitia mwongozo wa kitaifa wa ushiriki wa wananchi katika uwekezaji.
                                                                        PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU
                                                                         KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *