Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Umeme Wabadili Maisha ya Wananchi Ruvuma

Veronica Simba – Ruvuma

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme ameipongeza Serikali kwa kuunganisha umeme wa Gridi ya Taifa mkoani humo ambao umebadili hali ya maisha ya wananchi husika kutoka kwenye uduni na kuwa bora zaidi.

Ameyazungumza  hayo wakati akielezea hali ya upatikanaji wa umeme mkoani Ruvuma kwa Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani alipomtembelea ofisini kwake akiwa katika ziara ya kikazi, Desemba 12, 2019.

“Tunamshukuru sana Rais John Pombe Magufuli kwa kutuletea umeme, tangu nchi inapata Uhuru hatujawahi kupata umeme wa gridi lakini sasa hivi tunafurahia umeme kila uchao”, alisema Mndeme.

Akifafanua mabadiliko chanya yaliyoletwa na umeme kwa wananchi wa Ruvuma, Mkuu huyo wa Mkoa alisema yamejikita hasa katika shughuli za kimaendeleo.

Alisema, mashine za kusaga mahindi zilizokuwa zinatumia mafuta ya dizeli kwa kiasi kikubwa hazipo tena badala yake mashine nyingi sasa zinatumia umeme.

Alieleza zaidi kuwa uwepo wa mashine zinazotumia umeme kusaga nafaka kumepunguza kwa kiasi kikubwa gharama za kusaga nafaka hizo kwa wananchi ambao hutumia unga wa mahindi kupikia ugali.

Vilevile, alieleza kuwa vijiji vingi sasa vimekuwa na mwanga wa umeme hasa nyakati za usiku tofauti na ilivyokuwa awali.

Kufuatia suala hilo, aliipongeza serikali kwa kupitisha na kutekeleza azimio la kutobagua aina ya nyumba wakati wa kuunganisha umeme na kusema kuwa wananchi wengi wa maisha ya chini wanafurahia umeme kama wengine wenye kipato cha juu pasipo kujiona wametengwa.

Aidha, alishukuru kwa kazi inayoendelea ya kujenga miundombinu ya umeme ili kupeleka Gridi ya Taifa wilayani Tunduru huku akibainisha kuwa ndiyo wilaya pekee mkoani humo ambayo haijafikiwa na umeme huo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati alimweleza Mkuu huyo wa Mkoa kwamba kazi ya ujenzi wa miundombinu ya kupeleka umeme huo Tunduru imekamilika na kwamba katika ziara yake amejiridhisha na hilo.

“Wataalam wamefanya kazi nzuri sana na kwa sasa wanakamilisha kazi ndogo ndogo tu. Tunatarajia siku yoyote kuanzia hivi sasa, tutazima mitambo ya mafuta Tunduru na kuunganisha umeme wa Gridi ya Taifa”, alisema Kalemani.

Katika hatua nyingine, Waziri aliahidi kuwashawishi wawekezaji kwenda mkoani humo kufanya tathmini kwa ajili ya kuanzisha viwanda vya kutengeneza nguzo.

Alitoa ahadi hiyo kufuatia maombi ya Mkuu wa Mkoa ambaye alimweleza kuwa mkoa huo pia umejaaliwa kuwa na miti mingi hivyo ingefaa kukawa na kiwanda hicho ili kuunga mkono juhudi za serikali kutumia vifaa vya kuunganishia umeme ambavyo vinatengenezwa ndani ya nchi.

185 thoughts on “Umeme Wabadili Maisha ya Wananchi Ruvuma

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama