Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Ujenzi wa Barabara ya Kabingo – Kasulu – Manyovu Km 260 kwa Kiwango cha Lami Wanukia

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, ambaye amemwakilisha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isaack Kamwelwe, akihutubia Viongozi wa Serikali na wadau wa Sekta ya Ujenzi waliohudhuria katika warsha ya utambulisho wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu (km 260) sehemu ya Tanzania na Rumonge-Gitaza (km 45) sehemu ya Burundi kwa kiwango cha lami uliofanyika mkoani Kigoma.

Serikali ipo katika hatua za mwisho kuanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Kabingo – Kasulu hadi Manyovu yenye urefu wa kilomita 260 Kwa kiwango cha lami ikiwa ni hatua ya kuendelea kuufungua mkoa wa huo katika miundombinu ya barabara mkoani Kigoma.

Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara hiyo unatarajiwa kuwa wa muda mfupi kutokana na kugawanywa katika sehemu nne ambazo ni Manyovu – Kasulu (km 68.25), Kanyani – Mvugwe (km 70.5), Mvugwe – Nduta (km 59.35) na Nduta – Kabingo (km 62.50).

Akizungumza katika hafla ya kuutambulisha  mradi huo mkoani humo kwa viongozi wa Serikali ngazi ya mkoa, wadau wa Sekta ya Ujenzi na Wabunge,  Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, amesema tayari Serikali imepata fedha za mkopo wa nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo na kwamba kazi inayoendelea hivi sasa ni kukamilisha taratibu za kumpata mzabuni.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi wa barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu (km 260) kwa kiwango cha lami utakaoanza hivi karibuni. Ujenzi wa barabara hiyo utagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Alex Mubiru, akizungumza na Viongozi wa Serikali na wadau wa Sekta ya Ujenzi waliohudhuria warsha ya utambulisho wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu (km 260) sehemu ya Tanzania na Rumonge-Gitaza (km 45) sehemu ya Burundi kwa kiwango cha lami uliofanyika mkoani Kigoma.

“Mpaka sasa zabuni ya mradi wa barabara hii imeshatangazwa na ujenzi utaanza hivi karibuni mara baada ya taratibu nyingine kukamilika”, amesisitiza Mhandisi Mfugale.

Amebainisha kuwa mradi huu ni wa mfano kwani utahusisha miradi mingine ya kijamii inayogusa moja kwa moja wananchi katika Sekta ya Elimu, Maji na Afya.

Ametaja miradi hiyo kuwa ni Ukarabati wa masoko ya Makere na Manyovu, Ujenzi wa Sekondari ya Buhigwe na Shule ya Msingi Busunzu, Ujenzi wa vituo vya mabasi vya Manyovu na Kabingo, Kusambaza maji katika maeneo ya Busunzu, Kasulu, Buhigwe na Manyovu, Uboreshaji wa kituo cha Afya cha  Makere, Ununuzi wa magari manne ya Wagonjwa (Ambulance) na Ukarabati wa Hospitali ya Kasulu na Kibondo.

Akifungua warsha hiyo kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,  Prof. Joyce Ndalichako, amesema kuwa mradi huo ni moja ya miradi mikubwa ya Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaosaidia kuinua uchumi wa nchi sambamba na  kuunganisha mkoa wa Kigoma na mikoa mingine pamoja na nchi jirani.

“Mradi huu utaandika historia mpya katika nchi ya Tanzania kwani ni moja ya barabara pekee inayounganisha nchi yetu na nchi jirani iliyokuwa imebaki katika kiwango cha changarawe”, amesema Prof. Ndalichako.

Ameongeza kuwa utaratibu wa kuwafahamisha wadau na wananchi kuhusu ujio wa miradi utasaidia kutatua changamoto zitakazojitokeza na kupata ushirikiano wa karibu wa maoni ambayo yatawezesha kufanikisha utekelezaji wa mradi huo ndani ya muda, gharama na ubora unaotakiwa.

 

Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Uchukuzi na Mawasiliano) ambaye ni Mbunge wa jimbo la Muhambwe, Mhandisi Atashasta Nditiye (kulia), akiteta jambo na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako (kushoto), katika warsha ya utambulisho wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu (km 260) sehemu ya Tanzania na Rumonge-Gitaza (km 45) sehemu ya Burundi kwa kiwango cha lami uliofanyika mkoani Kigoma.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako, akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine wa Serikali pamoja na wadau wa Sekta ya Ujenzi kutoka nchi ya Tanzania katika warsha ya utambulisho wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu (km 260) sehemu ya Tanzania na Rumonge-Gitaza (km 45) sehemu ya Burundi kwa kiwango cha lami uliofanyika mkoani Kigoma.

Muonekano wa barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu (km 260) kwa kiwango cha lami utakavyokuwa mara baada ya ujenzi wake kukamilika, mkoani Kigoma. Ujenzi wa barabara hiyo utajumuisha miradi ya kijamii inayogusa moja kwa moja wananchi katika Sekta ya Elimu, Maji na Afya.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Naye Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Alex Mubiru, ameeleza kuwa Benki hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali na kuhakisha kuwa miradi hiyo inakuwa chachu ya kukua kwa uchumi na kupunguza umaskini.

Ameongeza kuwa Benki imeweza kuandaa fedha za utekelezaji wa miradi mikubwa mitatu (3) ambayo ni ujenzi wa barabara ya Kabingo-Kasulu-Manyovu (km 260), Dodoma Outer Ring (km 110.2) na ujenzi wa barabara Tanga – Pangani – Bagamoyo (km 121) ikiwa ni lengo la kufungua fursa mbalimali za maendeleo nchini Tanzania.

Warsha hiyo ya siku mbili yenye lengo la kuwafahamisha wadau mbalimbali kuhusu mradi huo imehusisha Mawaziri na Wabunge wanaotoka eneo la mradi, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa Wilaya zilizopo mkoani humo, Maafisa Watendaji wa Misitu, Madini, Ardhi, Shirika la Umeme (TANESCO), Maji na Shirika la Mawasiliano (TTCL).

103 thoughts on “Ujenzi wa Barabara ya Kabingo – Kasulu – Manyovu Km 260 kwa Kiwango cha Lami Wanukia

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama