Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

“Uhusiano wa Tanzania na Uganda ni mzuri sana” Rais Magufuli

Na. Immaculate Makilika- MAELEZO 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.  John Pombe Magufuli   amempongeza  na kumshukuru Rais wa Uganda, Yoweri Museveni   kwa kuwa miongoni mwa  viongozi wanaoendeleza fikra  za  Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ikiwa ni kielelezo cha  kuendeleza uhusiano mzuri ulipo baina ya nchi mbili za Tanzania na Uganda.

Akizungumza leo Ikulu jijini Dar es salaam, akiwa pamoja na mgeni wake Rais wa Uganda Yoweri Museveni ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, aliyewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja, Rais  Magufuli amemshukuru Rais Museveni kwa kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.

“Namshukuru Rais Museveni anaendeleza uhusiano wetu wa nchi hizi mbili, nataka niwaambie uhusiano wa Tanzania na Uganda ni mzuri sana” alisema Rais Magufuli.

Rais Magafuli alitaja masuala kadhaa waliyozungumza kuwa nia ni kuimarisha biashara kati ya nchi hizo mbili, ambapo alisema kuwa  kwa sasa biashara ya usafirishaji wa mizigo kwa njia ya treni kati ya Uganda na Tanzania imerejea baada ya kusimama kwa takriba miaka 10 na mzigo wa kwanza uliosafirishwa  ulikuwa na  uzito unaolingana na semitrela 40 hadi 50.

Aidha, alisisitiza kuwa “utandawazi ni mzuri katika biashara, lakini ni lazima tuangalie kwa upana na sheria zetu zizuie  changamoto zinazotokana na suala hilo”.

Akitolea mfano sukari ya ziada iliyoingizwa kinyemela katika masoko ya nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, ambayo haikutengenezwa nchini Uganda kama ilivyodaiwa hapo awali, Rais Magufuli alitahadharisha kuwa  tatizo hilo linaweza kuuwa viwanda vya ndani, pamoja na kupoteza ajira kwa wazawa wa nchi hizo.

Kwa upande wake, Rais Museveni, ambaye amekuja nchini kwa lengo la kumweleza  Rais Magufuli juu ya Mkutano wa Mataifa yanayoinukia kiuchumi (BRICS) uliofanyika mwezi uliopita huko nchini Afrika ya Kusini alisema kuwa aliwaelezea wafanyabishara wa nchi hizo juu ya fursa za uwekezaji zilizopo katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Ambapo, aliwataka wafanyabiashara hao kuja kuwekeza katika maeneo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na treni.

“Nilipata heshima ya kuzikaribisha kampuni zao zije kuwekeza huku Afrika Mashariki, kwani zitapata faida, kwa vile kiwango cha faida watakachopata huku ni kikubwa kuliko Ulaya, Asia na Amerika ya kusini” alisema Rais Museveni

Aidha, Rais Museveni alitaja utalii kama eneo lingine alilowataka wafanyabiashara hao wa nchi za BRICS kuja kuwekeza na kuongeza kuwa atafufua Shirika la Taifa la Ndege la Uganda ikiwa ni katika jitihada za kuimarisha sekta hiyo katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki.

Kuhusu masuala ya kikanda baina ya nchi na za Jumuiya ya Afrika Mashariki,   Rais Museveni alishukuru kuona Rais Magufuli amefufua usafirishaji wa mizigo kwa njia ya treni kutoka Dar es salaam hadi Mwanza na hatimaye kuvuka ziwa Victoria.

Aidha, alibainisha kuwa kusafirisha bidhaa kwa kutumia usafiri wa barabara  ni gharama, kuliko kutumia usafiri wa treni,  matokeo yake ni kuwa  bidhaa zilizosafirishwa kwa barabara zinakuwa na gharama ya juu kuliko zile zilizosafirishwa kwa treni.

Vilevile alibainisha kuwa changamoto zilizopo katika nchi za Burundi na Sudani ya Kusini zinaendelea kupatiwa ufumbuzi, ikiwa ni pamoja na wakimbizi kutoka nchi ya Burundi kurudi katika nchi yao.

Rais Museveni alikuwa nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja ambapo, amerejea nchini Uganda mara baada ya kumaliza ziara yake.


FacebooktwittermailFacebooktwittermail