Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Tunaungana na Ulimwengu Kuokoa Bahari- Tizeba

Sehemu ya fukwe wa Bahari ya Hindi maeneo ya Jiji la Dar es Salaam ikiwa imeathiriwa na uchafu. (Picha na Maktaba)

Na: Boss Brown

Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi  Dkt. Chares Tizeba ataongoza ujumbe kutoka Tanzania kushiriki  katika Kongamano la Bahari Duniani linalotarajiwa kuanza Jumatatu tarehe 5 hadi 9 katika  Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa New York nchini Marekani.

“Changamoto inayoikabili bahari ni kubwa kutokana na uchafuzi utokanao na taka sugu ambazo zinahatarisha uhai wa Bahari yetu, tunaunagana katika kushilikiana na wadau mbalimbali katika juhudi za kuiokoa bahari kwa pamoja.” Alisisitiza Tizeba.

Akifafanua amesema kama nchi wanachama tanaadhimia kutekeleza kipengele cha 14 cha Malengo ya Maendeleo Endelevu 17 ya agenda ya 2030 ya Umoja wa Mataifa Kinacholenga matumizi bora ya rasilimali za baharini.

Kongamano hili ni la muhimu  katika kuokoa bahari na litakutanisha Serikali, Umoja wa Mataifa, Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Mashirika yanayoshughulikia mazingira, Taasisi za elimu na wanasayansi ya Jamii, Asasi za Kirai, watu binafsi, makampuni na viwanda.

Miongoni mwa changamoto za ongezeko la taka sugu ni bidhaa zitokanazo na plastiki ambazo huchukua zaidi ya miaka 500 kuoza na kuathiri viumbe vya baharini na hata kuhatarisha afya za wanadamu. Hivyo wadau wanategemewa kutoa hatua mbadala za kusafisha bahari na kurudisha uhai wake kwa maisha ya baadaye.

Mambo mengine yatakayo jadiliwa katika kongamano hilo ni pamoja na kuongeza maeneo ya hifadhi baharini na kutunza rasilimali za bahari, kupunguza ongezeko la asidi itokayo viwandani inayoingia baharini; kudhibiti uvuvi haramu na kuweka mikakati ya kudhibiti uvuvi haramu; kuongeza elimu kwa jamii na utafiti wa kisayansi katika masuala ya bahari; kuongeza tija kwenye uchumi utokanao na baharini ambao hautakuwa na madhara makubwa kwa bahari pamoja na kutimizwa na kutekelezwa kwa sheria za kutumia bahari zilizowekwa na nchi wanachama.

Matokeo yaliyo tolewa na wanasayansi yanabainisha kwamba takriban  tani Million 8 za plasitiki huingia baharini ambapo kufikia 2050 kutakua na kiwango kikubwa cha plasitiki kuliko samaki na viumbe vingine vya baharini endapo hatua muhimu hazitachukuliwa kuiokoa bahari sasa.

Pamoja na changamoto zote hizi zote zinazoikabili bahari ipo nafasi ya kuokoa bahari kabla athari zaidi hazijajitokeza. Shirika la kusafisha fukwe duniani Ocean Conservancy kwa miaka 32 limekua likijishughulisha na kusafisha fukwe za bahari duniani kote, katika riporti yao ya mwaka 2015 wanaeleza kuwa “kuna matumaini endapo kwa pamoja tukiungana katika kutatua tatizo hili na kufikia Mpango wa Maendeleo Bora ya Agenda ya Mwaka 2030”.

Viumbe hai duniani kote kwa namna moja au nyingine maisha yao yote hutegemea bahari. Hewa unayovuta, maji unayokunywa, chakula unachokula, nguo unazovaa, magari tunayo tembelea n.k vyote hutegemea bahari kwa namna moja au nyingine. Bahari inatupa pia fulsa ya kupumzika, kustarehe, kuogelea, kucheza n.k.

“Kila mmoja ana mchango mkubwa sana katika harakati za kuiokoa kwani matatizo yanayoikabili bahari yamesababishwa na shughuli za wanadamu. Hivyo sisi wenyewe tuna uwezo wa kubadili mienendo ya maisha yetu ili kuiokoa bahari inayoelekea kutokomea”. Alisisitiza Tizeba

Siku moja kabla ya kuisha kwa kongamano hili alhamis ya tarehe 8 Juni pia kutaadhimishwa Siku ya Bahari Duniani ambayo ina kauli mbiu inayosema “Bahari Yetu Maisha Yetu” katika kuhamasisha jamii ya watanzania kuunga mkono kampeni ya ‘Okoa Bahari’. Ambapo Marafiki wa Bahari kutoka Tanzania watakusanyika katika fukwe za Bahari kufanya usafi ikiwa ni jitihada za kuunga mkono kampeni hii ya Kimataifa.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *