Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

TEWW yatakiwa Kupunguza Idadi ya Wasiojua Kusoma na Kuandika

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa kufungua mkutano wa nane wa Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima uliofanyika jana Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Dkt. Fidelis Mafumiko na Afisa Utumishi Bi. Mayasa Omary na kushoto ni viongozi wa vyama vya wafanyakazi.

Na Fatma Salum.

Serikali imetoa rai kwa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima nchini (TEWW) kuandaa mkakati wa kusaidia kupunguza idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika.

Rai hiyo imetolewa jana Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo wakati akifungua mkutano wa nane wa Baraza la Wafanyakazi la Taasisi hiyo.

Akizungumza na wajumbe wa Baraza hilo, Dkt. Akwilapo aliitaka TEWW kuandaa utaratibu mzuri wa kuwafikia wananchi wengi ambao hawajui kusoma na kuandika ili waweze kupata elimu kupitia taasisi hiyo.

Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo wakati wa mkutano wa baraza hilo uliofanyika jana Jijini Dar es Salaam.

“Ongezeko la wasiojua kusoma na kuandika linaelekea kuwa tatizo kubwa hapa nchini, hivyo natoa rai kwa taasisi hii kujadili namna ya kuendeleza kampeni za kisomo na kutoa mafunzo kwa wawezeshaji wa programu za kisomo ili kukabiliana na tatizo hilo.” Alisema Akwilapo.

Sambamba na hilo Dkt. Akwilapo aliwasisitiza watumishi wa taasisi hiyo kufuata sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa shughuli zake ili kufikia malengo waliyojiwekea na kuleta matokeo chanya kwenye sekta ya elimu nchini.

Aidha Katibu Mkuu huyo aliIshauri TEWW kuandaa utaratibu mzuri wa kuwasaidia kielimu wanafunzi wa kike walioshindwa kuendelea na masomo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kulazimishwa kuolewa au kupata ujauzito.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Dkt. Fidelis Mafumiko akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi hiyo katika mkutano uliofanyika jana Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Naibu Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Dkt. Kassim Nihuka na kulia ni watumishi wa taasisi hiyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Dkt. Fidelis Mafumiko alisema kuwa taasisi hiyo inashirikiana na wadau mbalimbali katika kuendesha programu za elimu kwa vijana na watu wazima walikosa elimu kupitia mfumo rasmi.

Alieleza kuwa program hizo ni pamoja na programu ya kuzuia ndoa za kulazimishwa za utotoni (Child Early and Forced Marriages) inayoendeshwa kwa kushirikiana na Taasisi ya Commonwealth of Learning ambayo imepanga kuwafikia walengwa 3000 katika mikoa ya Lindi, Rukwa na Dodoma.

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo (wa nne kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Dkt. Fidelis Mafumiko (wa nne kulia)  wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Taasisi hiyo katika mkutano uliofanyika jana Jijini Dar es Salaam.

Pia Dkt. Mafumiko alisema kuwa TEWW kwa kushirikiana na UNICEF wanaandaa programu kwa ajili ya vijana walio nje ya mfumo rasmi wa shule ikilenga kuwafikia vijana wapatao laki tano ndani ya miaka mitatu katika mikoa ya Tabora, Katavi, Geita, Rukwa, Dodoma, Simiyu, Shinyanga, Singida, Lindi na Manyara.

Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ilianza mwaka 1975 na ipo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na ina jukumu la kutoa mafunzo kwa wataalamu wa Elimu ya Watu Wazima na kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya watu katika jamii wakiwemo waliokosa fursa ya kupata elimu katika mfumo rasmi.

 

2 thoughts on “TEWW yatakiwa Kupunguza Idadi ya Wasiojua Kusoma na Kuandika

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama