Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

TBS Yashiriki Mikutano Ya Mashauriano Kati ya Serikali, Wafanyabiashara na Wawekezaji

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania akiongea wakati wa Mkutano wa Mashauriano kati ya Serikali, Wafanyabiashara na Wawekezaji Uliofanyika Mkoani Ruvuma

Na Neema Mtemvu

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limetoa elimu kuhusu fursa wanazopata wafanyabiashara na wazalishaji ambao bidhaa zao zimethibitishwa  ubora wake hivyo kuhamasisha wajasiriamali kuthibitisha ubora wa bidhaa zao bure pamoja na kuzipatia majibu changamoto wanazokumbana nazo wadau wake mbalimbali.

Shirika hilo limetoa elimu hiyo wakati wa mikutano ya mashauriano kati ya Serikali, wafanyabiashara na wawekezaji kwa ajili ya kusikiliza changamoto zinazowakabili kwenye mikoa ya Kusini ambayo ni Ruvuma, Mtwara na Lindi kuanzia Septemba 24, mwaka huu. Mikutano hiyo ilimalizika  mkoani Lindi.

Mikutano hii imehudhuriwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anjelina Mabula, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya  Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira),  Mussa Sima, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Anjellah Kairuki  wabunge na wakuu wa wilaya zote.

Akitoa mada kwa nyakati tofauti kwenye mikutano hiyo, Mkurugenzi wa TBS, Dkt. Yusuf Ngenya, aliwaeleza washiriki hao kuhusiana na mabadiliko ya sheria ya fedha ya mwaka 2019 ambayo yameleta mabadiliko katika Sheria ya Viwango Na: 2 ya mwaka 2009.

Kufuatia mabadiliko hayo, Dkt. Ngenya alisema shirika hilo kwa sasa linatekeleza baadhi ya majukumu ambayo awali yalikuwa chini ya iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) ambayo kwa sasa inajulikana kama TMDA.

Alisema kufuatia mabadiliko hayo majukumu ya kudhibiti ubora na usalama wa chakula na vipodozi yanafanywa na TBS.

Dkt. Ngenya alitaja huduma zinazotolewa na shirika hilo kwa sasa kuwa ni pamoja na usajili wa jengo, kusimamia masuala ya usalama na ubora wa chakula na vipodozi na upimaji wa bidhaa za vyakula na vipodozi kwa lengo la kudhibiti ubora na usalama .

Akieleza fursa zinazotolewa na shirika hilo kwa wajasiriamali nchini, Dkt. Ngenya, alisema ni pamoja kuthibitisha ubora wa bidhaa wanazozalisha bila malipo kwa miaka mitatu lengo likiwa ni kuwawezesha kupanua soko la bidhaa zao na kuwaondolea vikwazo vya kibiashara.

Alisema Serikali imeanzisha utaratibu huo ili kuwasaidia wajasiriamali kuzalisha bidhaa zenye ubora.

Alitoa wito kwa wajasiriamali na wananchi kwa ujumla kuichangamkia fursa hiyo hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inasisitiza uchumi wa viwanda.

“TBS kama taasisi wezeshi inatoa huduma ya kuthibitisha ubora wa bidhaa bure kwa wajasiriamali wadogo na wakati, lengo likiwa ni kuendeleza viwanda vya Tanzania, hivyo ni vyema wakathibitisha ubora wa bidhaa zao ili wasipate vikwazo vyovyote katika kupata soko ndani na nje ya nchi,” alisema Dkt. Ngenya.

Alisema kuwa endapo wajasiriamali hao watathibitisha bidhaa zao itawasaidia kuzalisha bidhaa endelevu ambazo zitakuwa na soko kila mahali ikiwemo masoko ya kikanda.

Dkt. Ngenya, alifafanua kuwa lengo la TBS ni kuwawezesha wafanyabiashara kufanya biashara zenye tija kwa taifa, bila kuathiri taratibu na sheria za nchi ndiyo maana shirika hilo limeshiriki mikutano hiyo kama taasisi wezeshi.

Mikutano hii ya mashauriano  kati ya serikali na wafanyabiashara wenye Viwanda, wawekezaji  ni utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa  Rais Dk John Pombe Magufuli aliyoyatoa mwezi Juni alipokutana na wafanyabiashara Ikulu Jijini Dar es salaam ambapo aliiagiza ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tamisemi pamoja na Wizara zote zinazohusika na wafanyabiashara, wawekezaji, wenye Viwanda nchini kwa lengo la kusikiliza kero na changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi

93 thoughts on “TBS Yashiriki Mikutano Ya Mashauriano Kati ya Serikali, Wafanyabiashara na Wawekezaji

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama