Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

TANESCO Ongezeni Nguvu ya Umeme Kwenye Vijiji Vyenye Uhitaji na Vyenye Viwanda Vidogo Vingi.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia) akisoma ujumbe uliowasilishwa kwake kwa njia ya mabango na wanakijiji wa kijiji cha Mwabakima katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa usambazaji wa umeme vijijini kupitia mradi wa kusafirisha umeme mkubwa wa 400kV backbone (BTIP) katika Wilaya hiyo.

Na Zuena Msuya, Tabora.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ameliagiza Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kuongeza ukubwa wa transifoma kutoka 100kV hadi kufikia 200kV katika kijiji cha Mwamashimba wilayani Igunga mkoani Tabora kutoka mahitaji makubwa ya umeme.

Mgalu alitoa maagizo hayo wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa usambazaji na kuwasha huduma ya umeme vijijini kupitia mradi wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa 400kV Backbone (BTIP) katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora pamoja na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa REA III awamu ya kwanza.

Mgalu alitoa maagizo hayo katika Kijiji cha Mwamashimba chenye mahitaji makubwa ya umeme baada ya  wanakijiji wengi kuanzisha viwanda vidogodogo zikiwemo mashine za kusaga na kukoboa nafaka, mashine za kukamua mafuta yatokanayo  na mbegu   pamoja kuwepo kwa shughuli nyingi za uchomeleaji vyuma.

“Hapa Mwamashimba  kunahitajika umeme zaidi maana watu wamejiajiri kwelikweli, wanafanya shughuli za maendeleo, hii ndiyo sera ya Serikali ya awamu ya tano, kwamba umeme uwafikie wananchi na uwanufaishe kwa kubadili maisha yao,transifoma mliofunga haiKidhi shughuli zao ni nyingi mnooo, TANESCO, hakikisheni mnaongeza transfoma nyingi walau wawe wanapata umeme wa 200kV, kutoka 100kV ya sasa, ili wahamasishe na vijiji vingine”, alisema Mgalu.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu(kulia) akizungumza na wanakijiji wa kijiji cha Jogohya katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa usambazaji wa umeme vijijini kupitia mradi wa kusafirisha umeme mkubwa wa 400kV backbone (BTIP) katika Wilaya hiyo.

Katika ziara hiyo, Mgalu aliwataka wananchi waliopitiwa na mradi wa BTIP kujiandaa kwa kusuka nyaya katika nyumba zao ili mkandarasi anapopita katika maeneo yao wawe tayari kuunganishwa na huduma hiyo kwa bei nafuu ya 27,000.

Aidha aliwatoa hofu wananchi wote wa maeneo husika kuwa  watapata huduma ya umeme kwa kuwa  tayari wakandarasi wamefanya upimaji na kuwa na ramani ya utekelezaji, usambazaji na uunganishaji wa umeme katika Vijiji vyote vilivyopitiwa na BTIP.

Vilevile aliwaasa wananchi  kuendelea kutunza na kuilinda miundombinu ya umeme zikiwemo nguzo  kwa kutoichoma moto, kutoiba vifaa mbalimbali ya miundombinu hiyo pamoja na kulima kwa njia salama katika majaruba.

Sambamba na hilo aliwataka wananchi hao pamoja na wakandarasi kushirikiana pamoja katika kutekeleza  mradi huo katika maeneo yao, pia wananchi wa eneo husika wapatie fursa ya ajira kulingana na uwezo wao wakati wa utekelezaji wa mradi huo.

Akiwa wilayani humo, Mgalu aliwasha huduma ya umeme katika vijiji vya Mwabakima ambapo 120 wanatarajia kunufaika kwa kuunganishwa huduma ya umeme katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa BTIP , wateja 35 kati yao tayari wameunganishwa na huduma  hiyo, Vilevile aliwasha huduma ya umeme katika kijiji cha Mwashimba ambapo wateja 150 wataunganishwa na huduma ya umeme katika awamu ya kwanza, 40 kati yao tayari wameshaunganishwa na huduma hiyo.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia) akimkabidhi kifaa cha umeme tayari (UMETA) mmoja wa akina mama wa kijiji cha Mwabakima katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa usambazaji wa umeme vijijini kupitia mradi wa kusafirisha umeme mkubwa wa 400kV backbone (BTIP) katika Wilaya hiyo.

Katika kijiji cha Jogohya, Mgalu alikagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo na kumtaka mkandarasi kutoka kampuni ya OK, kuharakisha kazi ya kujenga miundombinu kwa kuwa wananchi wengine wamekuwa wakiusubiri mradi huo kwa shauku kubwaa.

Katika hatua nyingine ,Naibu waziri huyo aliwataka wazazi, viongozi wa Serikali za mitaa pamoja vijijini, walimu pamoja na wakazi wa vijiji hivyo vya wilaya ya Igunga kuhakikisha wanapiga marufuku, wanapinga na kukataa kabisa ndoa za umri mdogo na mimba kwa watoto wadogo hasa wanafunzi.

Aliwaambia wananchi hao kuwa kila kaya ihakikishe inakuwa mlinzi wa mtoto wa Mwenzako, ili watoto hao hasa wasichana wapate fursa ya kusoma na baadaye hao hao Ndiyo watakaokuwa viongozi wa kesho na kuwaletea maendeleo hapo kijijini, huku akijitolea mfano yeye Mwenyewe kuwa endapo wazazi wake wangemuoza mapema je Leo hii angekuwa hapo alipo?


FacebooktwittermailFacebooktwittermail