Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Taarifa kwa Umma

Rais Magufuli apokea hati za utambulisho za Mabalozi wawili wa Japan na Georgia

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 19 Oktoba, 2018 amepokea hati za utambulisho za Mabalozi 2 walioteuliwa kuziwakilisha nchi za Japan na Georgia hapa nchini.

Mabalozi waliokabidhi hati zao za utambulisho ni Mhe. Shinichi Goto – Balozi wa Japan hapa nchini mwenye makazi Dar es Salaam Tanzania, na Mhe. Zurab Dvalishivili – Balozi wa Georgia hapa nchini mwenye makazi yake Addis Ababa Ethiopia.

Pamoja na kupokea hati zao za utambulisho Mhe. Rais Magufuli amesema Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na nchi hizo hasa kushirikiana katika uwekezaji, biashara, utalii na ujenzi wa miundombinu.

Mhe. Rais Magufuli amemueleza Balozi wa Japan hapa nchini Mhe. Shinichi Goto kuwa Tanzania na Japan zimeshirikiana katika utekelezaji wa miradi mingi ya ujenzi wa miundombinu na utoaji wa huduma za kijamii na kwamba anaamini ushirikiano huo utakuzwa zaidi kwa kuhakikisha miradi inayoendelea inakwenda vizuri na miradi mipya inaongezeka.

Mhe. Rais Magufuli amemueleza Balozi wa Georgia hapa nchini Mhe. Zurab Dvalishivili kuwa anatambua kuwa yeye ni Balozi wa kwanza kuteuliwa kuiwakilisha nchi hiyo hapa nchini, hivyo amemuomba awalete wawekezaji hasa wa viwanda kutoka Georgia kuja kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji huo.

Mabalozi hao wameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Tanzania ili kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano kati ya nchi zao na Tanzania.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

19 Oktoba, 2018


FacebooktwittermailFacebooktwittermail