Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Taarifa kwa Umma

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaratibu maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani, yatakayofanyika Jumatatu ya tarehe 01 Oktoba, 2018 ambapo wadau na wananchi watashiriki ikiwa ni pamoja.  Maadhimisho hayo yatatanguliwa na Salamu za Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William V. Lukuvi zitakazorushwa na Luninga ya TBC zikipeleka ujumbe huo kwa wananchi.

Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia makazi duniania (UN Habitat) hutoa kaulimbiu itakayoongoza tafakari ya kila mwaka. Mwaka huu, 2018 maadhimisho hayo yataongozwa na Kaulimbiu isemayo: “Managing Municipal Solid Waste”; Tafsiri ya kauli mbiu hiyo ni “Udhibiti wa takangumu kwenye Miji yetu”: Kauli mbiu hii inatuelekeza tutafakari namna tunavyoweza kuelimisha Umma kuhusu namna tunavyoweza kukusanya na kutupa taka ngumu kwa usahihi na kuepuka athari zinazoweza kusababishwa na mrundikano wa taka ngumu ambao ni changamoto ya miji mingi duniani.

Lengo kuu la maadhimisho haya ni kutoa mwongozo kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kutafakari kwa pamoja masuala yanayohusu miji, majiji na haki za msingi za wakazi katika miji yetu na kuangalia changamoto mbalimbali zilizopo ili kushirikishana mbinu na namna bora ya kutayarisha mikakati endelevu ya kupambana nazo.

Uzalishaji wa taka ngumu kutoka kwa wakazi wa mijini hukua kila siku na kusababisha mamlaka za upangaji na usimamizi wa miji kuingia gharama kubwa kuzikusanya, kuziondosha, na kuziteketeza. Aidha, ukusanyaji na uteketezaji wa taka ngumu uliozoeleka wa kutupa katika majalala ya taka (Dumping Sites)  na kuzichoma ama kuzifukia kumeleta athari nyingi za kiafya kwa wananchi waishio maeneo jirani zinazotokana na uchafuzi wa hewa (Air Pollution)  na uharibifu wa mazingira pia. Aidha, changamoto ya uchafuzi wa vyanzo vya maji umesababisha pia mlipuko wa magonjwa  yanayoenezwa kwa njia ya maji (Water borne Diseases) mfano kipindupindu (Cholera), kuhara / kuhara damu (dysentery) hususan wakati wa mvua.

Matokeo ya maadhimisho hayo ni matarajio ya kubuni njia mbadala na nyepesi za ukusaji na utupaji wa taka ngumu ambao utapunguza: gharama kubwa za ukusanyaji, usafirishaji na uteketezaji zinazoingiwa na mamlaka za miji; wenye kupunguza athari za kiafya na mazingira kwa wakazi wa mijini na wenye manufaa kwa jamii kama vile uzalishaji wa nishati na matumizi mengine ya kujirudia.

Tanzania inaungana na nchi nyingine ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Makazi Duniani kwa kufanya tafakari ikiongozwa na Kaulimbiu iliyotolewa na kushirikisha wadau muhimu ili kujadili namna bora ya kushughulikia changamoto ya uzalishaji na utupaji wa takangumu katika miji yetu. Mabadiliko ya tabia kwa kila mwananchi katika kuzalisha na kutupa taka ni muhimu na yanaweza kupunguza gharama kubwa zinazoingiwa na mamlaka za miji kuondosha takangumu na kupunguza athari zinazotokana na uwepo wa mrindikano wa taka hizo.

Baadhi ya nchi na miji duniani hutumia njia mbadala ya kutenganisha aina ya taka ngumu kuanzia zinapozalishwa ili kuweza kuzichakata na kurudia katika matumizi mengine (Recycling) ama kuzitumia kuzalisha nishati (Source of energy), ama kuzalisha vifaa na bidhaa zinazoweza kutumika katika ujenzi, bustani kama mbolea n.k.

Uthibiti wa taka ngumu kuanzia zinapozalishwa, zinaposafirishwa na zinavyoangamizwa kunaweza kubadili kabisa taswira ya miji yetu endapo mbinu za kisasa zitatumika kuzichakata na kutumika kama fursa badala ya kuwa kero kwa wakazi wa mijini. Baadhi ya watu wamejipatia kipato kutokana na taka ngumu (ukusanyaji chupa za plastiki, vyuma chakavu n.k.) huku miji yetu ikiendelea kupunguziwa kero ya taka hizo.

Siku ya Makazi Duniani huadhimishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kila Jumatatu ya kwanza ya Mwezi Oktoba. Chimbuko la maadhimisho ya Siku ya Makazi Duniani ni Azimio Namba 40/202 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililopitishwa mwezi Desemba mwaka 1985 na kuanza kuadhimishwa rasmi mwaka 1986. Mwaka huu maadhimisho hayo ya 33 yatafanyika Jijini Nairobi, nchini Kenya.

 

IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI

WIZARA YA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI.

30 thoughts on “Taarifa kwa Umma

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *