Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Taarifa kwa Umma

UWEKEZAJI KUTOKA CHINA KUTUFIKISHA UCHUMI WA KATI-MAJALIWA

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Jimbo la Jiangsu nchini China katika sekta ya kilimo na viwanda utaiwezesha nchi kufikia malengo yake ya kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka 2020 na ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Amesema  jimbo la Jiangsu ni miongoni mwa majimbo yaliyopiga hatua kubwa ya maendeleo kwenye teknolojia na viwanda duniani na Tanzania inahitaji wawekezaji wa uhakika katika sekta ya kilimo hususani watakaowekeza kwenye viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo, kuongeza thamani na kutafuta masoko.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana jioni (Jumatatu, Septemba 03, 2018) wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Gavana wa Jimbo la Jiangsu nchini China, Bw. Guo Yuan Qiung kwenye ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini China.

 “Tunathamini mchango wa Jimbo la Jiangsu katika uchumi wa Tanzania, ambapo sasa wawekezaji kutoka jimboni humo, waliowekeza kwenye viwanda mbalimbali kama cha kuchambua pamba, kutengeneza nyuzi na kukamua mafuta ya kula kwa kutumia mbegu za pamba cha Jielong kilichopo wilayani Shinyanga na kiwanda cha nguo cha Urafiki cha jijini Dar es Salaam.”

Kadhalika, Waziri Mkuu alisema bado mchango wa jimbo hilo unahitajika katika uendelezaji viwanda hususan katika masuala ya teknolojia ya viwanda, kuimarisha utafiti kwenye sekta ya kilimo na kuisaidia Tanzania kupata masoko ya mazao kama mbaazi, muhogo na soya. “Tunaomba uendelee kuhamasisha kampuni nyingi zaidi kutoka jimboni kwako kuja kuwekeza nchini.

Kuhusu kiwanda cha nguo cha Urafiki cha jijini Dar es salaam, Waziri  Mkuu na Naibu Gavana huyo walikubaliana kuangalia uwezekano wa kufanya mapitio ya changamoto  za uendeshaji wa kiwanda hicho ili kutafuta suluhisho la mapungufu yanayojitokeza katika kiwanda hicho.

Kwa upande wake, Bw. Qiung alimhakikishia  Waziri Mkuu ushirikiano wa hali ya juu  hasa katika uwekezaji wa viwanda na kwamba anaamini kuwa mkutano wa FOCAC utatoa dira ya   maendeleo kwa Tanzania na Bara zima la Afrika.

Aliongeza kuwa  jimbo lake lipo tayari kushirikiana na Tanzania katika masuala ya elimu kwani lina vyuo vingi vinavyotoa kozi mbalimbali na aliwakaribisha wanafunzi kutoka Tanzania kwenda jimboni humo kusoma.

 IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMANNE, SEPTEMBA 04, 2018.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *