Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete akikagua samani zilizowekwa katika Jengo la Tatu la Abiria (TBIII) katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Atupele Mwakibete, ameitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kushirikiana kwa karibu na taasisi zote za Serikali na zisizo za Serikali zinazotoa huduma katika viwanja vya ndege ili kuboresha utoaji wa huduma viwanjani.
Amesema hayo jijini Dar es Salaam mara baada ya kukagua jengo la tatu la abiria katika kiwanja cha ndege cha Kiimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), na kusisitiza ushirikiano utaboresha huduma na kuongeza mapato.
“Viwanja vya ndege vya Julius Nyerere (JNIA), KIA, Mbeya, Mwanza, Dodoma na Arusha ambavyo kwa sasa vina idadi kubwa ya abiria wanaoingia na kutoka endeleeni kuongeza ubunifu”, amesema Mhe. Mwakibete.
Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, akisisitiza jambo kwa viongozi wa Mamlaka ya VIwanja vya Ndege Tanzania (TAA), alipokagua Jengo la Tatu la Abiria (TBIII), katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri huyo amesema uimarishaji wa utoaji wa huduma viwanjani unategemea ushirikiano wa karibu wa wadau ambao utaongeza imani ya mashirika mbalimbali ya ndege ndani na nje ya nchi na hatimaye kuongeza mapato.