Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Serikali Yawahakikishia Wananchi Kuwa EFD Zitaendelea Kufanya Kazi Wakati Wowote Kuanzia Sasa.

 

Na Frank Mvungi 

Serikali imewahakikishia Wananchi kuwa inafanya juhudi za maksudi kuhakikisha kuwa changamoto iliyojitokeza  katika mashine za kutolea risiti za  Kielekroniki (EFD) inapatiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo ili wananchi waendelee kupata huduma hiyo.

Akitoa maelezo hayo leo Bungeni Jijini Dodoma  kufuatia hoja iliyotolewa na Mbunge wa Sumve Mhe. Richard Ndasa, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa changamoto ya mashine  hizo kushindwa kufanya kazi inatatuliwa haraka iwezekanavyo.

“Wataalamu wa Wizara ya Fedha, TRA na Wakala ya Serikali Mtandao wanashirikiana kuhakikisha kuwa wanatatua changamoto ya mfumo wa mashine hizi kutokufanya kazi. Matumaini yetu ni kuwa watakamilisha kazi hii mapema iwezekanavyo,”  alisisitiza  Kijaji

Dkt. Kijaji amesema, ni kweli kuwa tatizo hilo lilijitokeza na Serikali ilichukua hatua za kurekebisha changamoto hiyo na baadae lilijitokeza tena na Serikali kupitia wataalamu wake inaendelea kufanya juhudi za kuitatua.

Aidha, Mbunge wa Sumve Mhe. Richard Ndasa alitaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali kutokana na mashine za kutolea risiti za EFD kushindwa kufanya kazi kwa muda wa zaidi ya wiki moja sasa na kuliomba Bunge kujadili jambo hilo ambapo Serikali imeeleza hatua zinazochukuliwa kutatua changamoto hiyo.

Matumizi ya Mashine za Kielektroniki katika kutoa risiti yamechagiza kuongezeka kwa mapato ya Serikali na kuimarisha wigo wa ukusanyaji mapato hali inayochochea ustawi wa huduma kwa wananchi na maendeleo kwa ujumla.


FacebooktwittermailFacebooktwittermail