Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Serikali yatoa Ajira zaidi ya 1,666 Ndani ya Utumishi wa Umma

 

Serikali ya awamu ya tano imeendelea kutekeleza kwa vitendo ahadi yake ya kutoa fursa za ajira kwa Watanzania wenye sifa, ujuzi na elimu katika ngazi mbalimbali kadri ya mahitaji kwa lengo la kuongeza rasilimali watu serikalini ili kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi.

Kati ya mwezi Machi na Aprili, 2019 zaidi ya nafasi wazi za kazi 1,666 zimetangazwa na Serikali kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Akiongea na wadau mbalimbali waliomtembelea ofisini kwake leo, Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Xavier Daudi aliwaeleza kuwa nafasi hizo ambazo mchakato wake upo katika hatua mbalimbali ni kwa ajili ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) nafasi 338, madereva 851 kwa ajili ya Wizara, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi nyingine za Serikali, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) nafasi 50, Mamlaka ya Viwanja vya ndege nafasi 119, Mamlaka ya mafunzo ya ufundi stadi (VETA) nafasi 43.

Taasisi zingine za serikali ambazo zinatarajiwa kupata watumishi wapya ni Chuo cha Taifa cha Usafirishaji nafasi 26, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) nafasi 25 na Chuo cha Elimu ya Biashara nafasi 19.

Aliongeza kuwa nafasi nyingine ni kwa ajili ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka nafasi 16, Wizara ya Afya nafasi 14, Wakala wa huduma za misitu nafasi 11, Shirika la Elimu Kibaha nafasi 9, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) nafasi sita, Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) nafasi tano, Bohari Kuu ya Dawa (MSD) nafasi tatu, Mamlaka ya Uendelezaji wa Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KADCO) nafasi mbili, Baraza la Taifa la Ujenzi NCC) nafasi mbili, Taasisi ya Utafiti wa Chai (TRIT) nafasi moja, Wakala wa Umeme Vijijini (REA) nafasi 1, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Rufaa ya Ununuzi wa Umma (PPAA) nafasi moja, Hospitali ya Benjamini Mkapa nafasi 1, Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi (MUHAS) nafasi moja, Wakala wa Ndege za Serikali nafasi moja na Taasisi ya Bahari Dar es Salaam nafasi moja.

Aidha matangazo hayo yote utekelezaji wake uko katika hatua mbalimbali kulingana na tarehe za kila tangazo.

Daudi aliongeza kuwa jumla ya nafasi wazi za kazi 146 za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambazo usaili wake ulifanyika mwezi machi, majina ya waombaji kazi waliopangiwa kituo cha kazi yanatarajiwa kutolewa hivi karibuni.

Katibu huyo amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano ni Serikali inayolenga kuwa na watu wenye sifa stahili ili kuiwezesha Tanzania kufikia kwenye uchumi wa kati kwa haraka na ndio maana imeendelea kutoa vibali vya ajira katika maeneo mbalimbali ili kuongeza rasilimaliwatu katika kusukuma utekelezaji wa mipango na mikakati mikubwa ya Serikali kwa faida ya taifa.

Bwana Daudi    amefafanua kuwa kuwa ofisi yake imeendelea kubuni mifumo mbalimbali ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi wa kazi. Mifumo hiyo mipya imesaidia kurahisisha uendeshaji wa mchakato wa ajira kwa haraka kwa kuzingatia kuwa idadi ya waombaji kazi ni kubwa hivyo pamoja na rasilimaliwatu aliyokuwa nayo lakini matumizi ya mifumo ya TEHAMA hasa ‘recruitment portal’ imeendelea kurahisha mchakato wa ajira kwa kila nafasi za kazi zinapotangazwa.

“Niwahakikishie kuwa tumeendelea kuboresha huduma zetu za uendeshaji wa mchakato wa ajira kwa kubuni na kuboresha mfumo wa upokeaji wa maombi ya kazi “recruitment portal” mfumo wa kupangia watu kazi kupitia kanzidata (Placement Management Information System).

Mifumo hii imeongeza uwazi zaidi kwa wateja na wadau wetu kuliko hapo awali, Shabaha yetu ni kufanya kazi kwa malengo hasa kwa kutumia mifumo hii kupata watumishi bora kwa haraka ili kuongeza nguvu ya rasilimaliwatu kwa waajiri na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi” alieleza Daudi.

 

112 thoughts on “Serikali yatoa Ajira zaidi ya 1,666 Ndani ya Utumishi wa Umma

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama