Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Serikali ya Awamu ya Tano Yaleta Mageuzi MOI

 Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya MOI Mama Zakia Meghji akifafanua jambo kwa wajumbe wa Bodi hiyo wakati wa kikao chake leo Jijini Dar es Salaam.

Na; Mwandishi wetu

Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini MOI Mama Zakia meghji leo amewaongoza wajumbe wa bodi hiyo kupitia na kupitisha mikakati na mipango mbalimbali inayolenga kuboresha huduma kwa wagonjwa kuelekea maadhimisho ya miaka 3 ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Mama Meghji amesema, Taasisi ya MOI ni tegemeo kubwa kwa watanzania na nchi nyingi za Afrika hivyo ni muhiumu kuendelea ketengeneza mbinu za kimkakati za kuendelea kutoa huduma bora, kuanzisha huduma mpya za matibabu na kutekeleza kwa vitendo agizo la Mh Rais Dkt John Pombe Magufuli la kuhakikisha huduma zote za afya zinapatikana hapa nchini na hivyo kufuta rufaa za kupeleka wagonjwa nje ya nchi ambazo zimekua zigharimu Serikali fedha nyingi.

Katibu Mtendaji wa Bodi ya wadhamini ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respiciopus Boniface akifafanua jambo wakati wa kikao cha Bodi hiyo leo Jijini Dar es Salaam.

“Nafahamu sasa tunakwenda vizuri, Serikali imetuwezesha tumekuwa na vifaa vya kisasa kabisa, tuna MRI ya kisasa sawa na ile inayotumika huko ulaya, tuna CT SCAN ya kisasa pia,tuna X-ray za kidigitali hivyo ni muhimu kuendelea kujipanga kuboresha huduma zetu. Naamini MOI ni bora lakini ni lazima kuboresha zaidi”. Alisema Mama Meghji

Mama Meghji amesema, pamoja na mambo mengine kikao hiki kimepitia taarifa ya mfumo wa upimaji wa wazi wa watumishi yaani OPRSAS pamoja na masuala mengine yanayolenga kuboresha huduma.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface amesema, Taasisi ya MOI iko kwenye mageuzi makubwa ya utoaji wa huduma zake hapa barani Afrika ambapo siku za hivi karibuni wananchi wengi kutoka mataifa jirani wamekuwa wakifika MOI kupata huduma, hivyo lazima huduma ziboreshwe ili waendelee kupata huduma stahiki na kwa wakati.

Katikati ni Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini MOI Mama Zakia Meghji, Kushoto kwake ni Mjumbe wa bodi hiyo Profesa Bakari Lembariti na Kulia ni Mkurugenzi mtendaji wa MOI Dkt Respicious Boniface wote wakipitia nyaraka mbalimbali zilizowasilishwa kwenye kikao hicho.

“Ni ukweli usiopingika kwamba, huduma zetu zimeboreka sana katika kipindi cha miaka 3 ya Serikali ya awamu ya 5 inayoongozwa na Dkt John Pombe Magufuli, tuna vifaa vya kisasa  kabisa hivyo ni muhimu sisi viongozi kukutana na kuhakikisha tunaboresha huduma kadri iwezekanavyo” Alisema Dkt Boniface.

Dkt. Boniface anasema Taasisi ya MOI imepata vifaa vya kisasa hivyo ni muhimu kukutana na kutengeneza mikakati  ya kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani kwa kuleta wataalamu kutoka mataifa mbalimbali ili huduma zote ziendelee kutolewa hapa nchini ambapo hivi karibuni Taasisi ya MOI itakuwa mwenyeji wa kongamano la kimataifa la madaktari wa Ubongo, Mgongo na mishipa ya fahamu.

Vikao vya bodi ya wadhamini MOI vimekua vikifanyika kila baada ya miezi 3 kwa lengo la kufanya tathmini ya hali ya utoaji huduma na kuhakikisha changamoto zote zilizojitokeza katika kipindi hicho zinatatuliwa.

(Picha zote na Habari MOI)

 


FacebooktwittermailFacebooktwittermail