Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Serikali Kujenga Kingo Maeneo Yanayozungukwa na Maji

Na Lilian Lundo.

Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira imeanzisha miradi ya kujenga kingo katika maeneo yanayozungukwa na maji ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. January Makamba jana  katika kipindi cha Tunatekeleza kinachorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC) na kuratibiwa na Idara ya Habari (MAELEZO).

“Ujenzi wa kingo katika Bahari ya Hindi kumesaidia bahari kutoichukua barabara kwa zaidi ya miaka 70 ijayo,” alisema Makamba.

Aidha, Makamaba amesemawameanzisha mifumo mbalimba itakayowezesha kukagua viwanda na kuwaelekeza wenye viwanda juu ya utunzaji wa mazingira ikiwemo kuongeza idadi ya wakaguzi wa mazingira.

Amesema, kitu kikubwa ambacho Serikali ya Awamu ya Tano inajivunia ni kuondoa viroba nchini kwani vilikuwa vikichafua mazingira kwa kiasi kikubwa. Vile vile imeteua wakaguzi wa mazingira ambao watahakikisha wanazuia matishio ya mazingira yanayotokea mara kwa mara.

Makamba amesema, ushirikiano wa Zanzibar na Tanzania Bara haupo tu katika sekta za kimuungano bali zinashirikiana vizuri hata katika sekta zisizo za Muungano

Hata hivyo, Ofisi ya Makamu wa Rais  ipo katika hatua ya mwisho ya kuifanyia mapitio Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 1997 kutokana na sera hiyo kupitwa na wakati, hivyo iweze kujumuisha changamoto mpya zilizojitokeza  ikiwa ni pamoja na ongezeko la kemikali za sumu taka zinazotokana na vifaa vya kie-elekroniki, masuala ya matumizi ya bioteknolojia ya kisasa, mabadiliko ya tabia nchi, viumbe vamizi na masuala ya biofueli.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *