Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Serikali  Kuanzisha Vituo Maalum vya Kuuzia Mazao

Na Georgina Misama

Serikali imepanga kuanza matumizi ya vituo maalum vya kuuzia mazao ili kuwasaidia wakulima kudhibiti ubora wa mazao yao, kupata taarifa za masoko na kuimarisha ushindani wa bei.

Makubaliano ya matumizi ya vituo hivyo yamefikiwa na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia Bodi ya Usimamizi Stakabadhi za Ghala na Halmashauri za maeneo yanayotekeleza Mfumo wa stakabadhi.

Akizungumza leo Bungeni wakati wa kuwasilisha bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2017/18, Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage amesema kwamba serikali inahamasisha ushindani kwa kutumia vituo maalum na Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ambao umefanikisha uuzaji wa mazao kwa uwazi na hivyo kumpatia mkulima bei shindani.

“Utaratibu huo umewezesha bei ya Korosho kupanda na kufikia wastani wa Shilingi 3,880 kwa kilo msimu wa 2017/2018 ikilinganishwa na Shilingi 3,346 kwa kilo msimu wa 2016/2017 hivyo mfumo huu ni bora ukilinganisha na utaratibu wa awali” alisema Mwijage.

Aidha, mauzo ya Korosho kupitia Mfumo huo yameongezeka kutoka tani 249,912 msimu wa 2016/2017 hadi tani 291,614 msimu wa 2017/2018 sawa na ongezeko la asilimia 16.7.

Mwijage amevitaja vituo ambavyo vinaendelea kuboresha utendaji wake kuwa ni vya mipaka ya Holili/Taveta, Sirari/Isebania,  Namanga/Namanga, Kabanga/Kobero, Rusumo/Rusumo, Mutukula/Mutukula pamoja na Horohoro/Lungalunga.

Aidha, ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Mpakani cha Tunduma/Nakonde upande wa Tanzania ulioanza mwezi Novemba 2016, unatarajiwa kukamilika mwezi Mei 2018. Hadi kufikia mwezi Februari 2018 ujenzi wa kituo hicho umefikia asilimia 75.

Katika kuboresha mazingira ya kufanya biashara za mazao nchini, serikali kupitia taasisi husika chini ya Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji imeendelea kutoa elimu kwa umma ili kujua umuhimu wa kutumia vituo maalum vya kuuzia mazao.

Wakati huo huo Waziri Mwijage ameliambia Bunge kuwa, katika kuhakikisha Tanzania ya viwanda inawezekana mwongozo wa kusimamia ujenzi wa viwanda katika mamlaka za tawala za mikoa umekamilika.

Aidha viwanda vipya 3306 vikubwa na vidogo vimejengwa katika kipindi ambacho serikali ya awamu ya tano imeingia madarakani hadi Machi 2018, pia wizara inaendelea kuandaa na kuhakikisha kunakuwa na mazingira wezeshi ya kufanya biashara ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi hasa katika sekta ya Kilimo.

 

73 thoughts on “Serikali  Kuanzisha Vituo Maalum vya Kuuzia Mazao

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *