Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Serikali Imeipa Kipaumbele Sekta ya Michezo Nchini ili Kutoa Ajira Kwa Vijana

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza akifungua mashindano ya pili ya mchezo wa Taekwondo yanayofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 14-15 Disemba, 2019 mwishoni mwa wiki katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Na Eleuteri Mangi, WHUSM, Arusha

Serikali ya Awamu ya Tano imeipa kipaumbele sekta ya michezo nchini kwa kuweka mikakati inayohakikisha michezo yote ikiwemo Taekwondo inafanya vizuri ili kuwa chanzo cha kutoa ajira kwa vijana pamoja na kukuza uchumi wa taifa.

Akifungua mashindano ya Taekwondo ya pili ya mchezo wa yanayofadhiliwa na Ubalozi wa Korea nchini kwa mwaka 2019 kwa nchi za Afrika ya Mashariki yanayofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha mwishoni mw wiki, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza alisema kuwa  Serikali inatambua umuhimu wa michezo yote nchini ikiwemo mchezo wa Taekwondo.

Akijibu moja ya maombi yaliyotolewa na Rais wa Shirikisho la Mchezo wa Taekwondo nchini (TTF) Ramoudh Ally la kupatiwa eneo la kujenga uwanja mkubwa wa ndani wa kisasa kwa ajili ya mchezo wa Taekwondo wakati akitoa historia ya mchezo huo nchini, Naibu Waziri alisema kuwa kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya michezo nchini ya mwaka 1995 jukumu la kusimamia na kuendeleza sekta ya michezo ni la Serikali, jamii nzima pamoja na wadau mbalimbali ukiwemo Ubalozi wa Korea nchini.

Balozi wa Jamhuri ya Watu wa Korea Taekwondo Cho Tae-ick (kushoto) akiteta jambo na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza (kulia) wakati wa ufunguzi wa mashindano ya mchezo wa Taekwondo yanayofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 14-15 Disemba, 2019 mwishoni mwa wiki katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

 “Natoa wito kwa wadau wa michezo kuendelea kushirikiana na Serikali kukuza, kuendeleza na kuwekeza katika sekta ya michezo nchini ikiwemo mchezo wa Taekwondo, kwani Serikali ipo tayari kushirikiana na wadau mbalimbali kuendeleza michezo ikiwemo Ubalozi wa Jamhuri ya Watu wa Korea nchini ili kuhakikisha sekta hii inakuwa na tija kwa jamii na taifa zima” alisema Naibu Waziri Shonza

Aidha, ameataka maafisa michezo nchini kuanzia ngazi ya mikoa na wilaya kushirikiana na viongozi wa Mashirikisho na Vyama vya Michezo ili kuhakikisha vyama na vilabu ambavyo havijapata usajili kupitia Baraza la Michezo nchini (BMT) ambalo limepewa dhamana ya kusajili mashirikisho, vyama na vilabu hapa nchini.

Kwa upande wake Balozi wa Jamhuri ya Watu wa Korea nchini Cho Tae-ick ambaye ofisi yake ni mdhamini wa mchezo huo amesema kuwa mchezo wa Taekwondo unafaida nyingi na unachezwa na watu wa rika zote kuanzia watoto wadogo hadi watu wazima kwa kuimarisha na kujenga mwili ambapo husaidia kuimarisha umakini katika kutimiza majukumu yao ya kila siku.

Balozi wa Jamhuri ya Watu wa Korea nchini Cho Tae-ick ambaye ofisi yake ni mdhamini wa mchezo wa Taekwondo akiongea wakati wa ufunguzi wa mashindano ya mchezo wa Taekwondo yanayofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 14-15 Disemba, 2019 mwishoni mwa wiki katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha. Aliyeketi katikati ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza na Rais wa Shirikisho la Mchezo wa Taekwondo Tanzania (TTF) Ramoudh Ally (kulia).

Balozi huyo ameendelea kuzitaja faida nyingine za mchezo huo kwa ni kuwajengea uwezo wachezaji wa kujilinda kiusalama, kuwafundisha saikolojia ya namna bora ya maisha pamoja na kuwajengea urafiki miongoni mwa wachezaji.

“Taekwondo ni mchezo mzuri sana, kila kitu katika mwili wa binadamu ni silaha ya kujikinga, cha msingi ni kujua namna ya kuitumia kwa faida kwa jamii nzima, elimu hiyo inapatikana katika mchezo wa Taekwondo” alisema Balozi Cho.

Awali akitoa historia ya mchezo wa Taekwondo nchini Rais wa Shirikisho la mchezo huo nchini (TTF) Ramoudh Ally alisema kuwa Taekwondo ni mmoja kati ya michezo inayotambuliwa na Baraza la Michezo Tanzania pamoja na Kamati ya Olympic duniani.

Mchezo Taekwondo nchini ulianza kutambuliwa rasmi mwaka 2003 na Shirikisho la Taekwondo duniani ambalo makao yake makuu yapo nchini Korea ya Kusini ambapo hadi sasa Tanzania ni mwanachama hai na inashughulika na masuala yote ya mchezo huo duniani.

Wanamichezo wa mchezo wa Taekwondo wakiendelea na mashindano ya mchezo huo wakati wa ufunguzi wa mashindano yanayofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 14-15 Disemba, 2019 mwishoni mwa wiki katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

Mashindano Taekwondo ya mwaka 2019 yanayojulikana kama “Korean Ambassador’s Cup” ni ya pili kufanyika nchini ambapo hufanyika kila baada ya miaka miwili kwa mara ya kwanza yalifanyika mwaka 2017. Mashindano ya mwaka huu yanafanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 14 hadi 15 Disemba 2019 jijini Arusha ambayo yanajumuisha jumla ya washiriki 172 kutoka katika nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Kenya, Rwanda, Uganda na mwenyeji Tanzania pamoja na washiriki kutoka nchini Malawi.

Baadhi ya mashabiki waliohudhuria ufunguzi wa mashindano ya mchezo wa Taekwondo yanayofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 14-15 Disemba, 2019 mwishoni mwa wiki katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

179 thoughts on “Serikali Imeipa Kipaumbele Sekta ya Michezo Nchini ili Kutoa Ajira Kwa Vijana

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama