Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Sekta ya Madini Yakua kwa Asilimia 17.5 kwa Mwaka 2017.

 

Na: Lilian Lundo 

Sekta ya madini imekua kwa asilimia 17.5 ikilinganishwa na asilimia 11.5 ya mwaka 2016 ambapo ongezeko hilo limetokana na kuimarishwa kwa udhibiti  wa biashara haramu na utoroshwaji wa madini, kuimarishwa kwa ukaguzi na usimamizi katika sehemu za uzalishaji, biashara ya madini pamoja na usafirishaji wa madini nje ya nchi.

Waziri wa Madini, Mhe. Angellah Kairuki amesema hayo leo, Bungeni Jijini Dodoma alipokuwa akiwasilisha mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2018/2019.

“Ukuaji wa sekta ya madini pia kumetokana na kuongezeka kwa viwango vya mrabaha na kuanzishwa kwa ada ya ukaguzi wa madini kufuatia marekebisho ya sheria ya madini ya mwaka 2010 yaliyofanyika mwaka 2017 na kanuni zake,” amesema Mhe. Angellah Kairuki.

Aidha amesema, mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa umeendelea kuimarika ambapo katika mwaka 2017 mchango huo ulifikia asilimoa 4.8. Kwa upande wa thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi, mauzo yalifikia Dola za Marekani 1,810,697,000 mwaka 2017.

“Ni matarajio yetu kuwa thamani ya mauzo inaendelea kuongezeka tena baada ya kukamilisha mageuzi makubwa ambayo tuliyaanzisha ikiwa ni pamoja na uongezaji thamani madini ndani ya chini,” amesema Mhe. Kairuki.

Waziri Kairuki amezitaja kazi zilizopangwa kutekelezwa kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 na Wizara ya Madini na Taasisi zake kuwa ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali yatokanayo na rasilimali madini, kuwaendeleza wachimbaji wadogo na wa kati wa madini pamoja na kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini.

Amezitaja kazi nyingine kuwa ni kuimarisha ufuatiliaji wa ukaguzi wa usalama, afya, mazingira na uzalishaji wa madini katika migodi midogo, ya kati na mikubwa, kuendelea kuhamasisha uwekezaji katika miradi ya kimkakati ya Sekta ya Madini, kuendelea kuboresha mazingira ya kuwawezesha wananchi kufaidika na rasilimali madini, kuelimisha Umma na kuboresha mawasiliano kati ya Wizara na wadau mbalimbali kuhusu masuala ya madini.

Vile vile kusimamia, kufuatilia na kuboresha sera, sheria, kanuni, mikakati na miongozo mbalimbali ili kuleta ufanisi na tija katika sekta ya madini, kuendeleza rasilimali watu na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na kuwezesha Taasisi zilizo chni ya Wizara.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe. Dunstan Kitandula amesema Serikali iangalie namna bora ya kuwezesha Wakala wa Jiolojia nchini ili iweze kufanya tafiti za madini yote nchini nakuwa na Kanzi Data ambayo itatumiwa na wawekezaji toka nje, ambapo itapunguza athari kubwa za kimazingira zinazosababishwa na watafiti kutoka nje ya nchi ambao wakimaliza tafiti zao nchi hainufaiki na tafiti zilizofanywa kwenye rasilimali zake.

Wizara ya Madini imeomba kuidhinishiwa na Bunge mapendekezo ya Bajeti ya Fungu 100 la Wizara hiyo jumla ya shilingi 58,908,481,992 kwa ajili ya matumizi ya Wizara na Taasisi zake kwa mwaka wa Fedha 2018/2019.

 

 

 


FacebooktwittermailFacebooktwittermail