Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Sekta Binafsi Yachangia Maandalizi Wiki ya Tanzania Nchini Kenya

Na Jonas Kamaleki

Serikali itadumisha ushirikiano na sekta binafsi katika kutafuta fursa za kibiashara katika soko la pamoja la Afrika Mashariki na maeneo mengine duniani ili kujenga uchumi.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga wakati akipokea michango ya wadau toka sekta binafsi kwa ajili ya kufanikisha maandalizi ya wiki ya Tanzania nchini Kenya.

“Ninawashukuru sana kwa ushirikiano wenu na kuonyesha uthubutu wa kuingia katika soko la Kenya, ninyi ni mabalozi wa wafanyabiashara wengine katika kutafuta fursa za kibiashara nje ya Tanzania”alisema Balozi Mahiga.

Balozi Mahiga alisema Tanzania inazobidhaa nyingi za viwanda ambazo nchi nyingine hawazijui bidhaa hizo, hivyo kinachofanywa na sekta binafsi kushirikiana na Serikali jambo la kijivunia.

Aidha, Balozi Mahiga alisema kuwa kufanya biashara nje ya nchi kunaimarisha uhusiano wa kisiasa baina ya Serikali ya Tanzania na nchi nyingine na kukuza diplomasia ya uchumi.

Aliongeza kuwa hii ni fursa kwa ajili ya ujenzi wa uchumi wa viwanda ambao ni msisitizo na mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Waliotoa michango yao ni Kampuni ya Konyagi ambao wamechangia shilingi milioni 11, Mohamed Enterprises, Shilingi milioni 25 na NIDA TEXTILE MILLS (T) LTD imetoa hundi ya shilingi milioni 22.

Balozi Mahiga amewaomba wafanyabiashara wengine wajitokeze kuchangia na kushiriki katika fursa hiyo ya kutafuta masoko nje ya nchi hususan Kenya ambapo bidhaa za Tanzania zitaoneshwa huko kuanzia tarehe 25 hadi 28, Aprili, 2018.

Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Rehema Mtingwa, amesema sekta binafsi iko tayari kushirikiana na Serikali katika kufanikisha upatikanaji wa fursa za kibiashara nchini Kenya na sehemu nyingine.

Hii ni mara ya pili kwa wadau toka sekta binafsi kuchangia maandalizi hayo, kundi la kwanza ambalo lilijumuisha KNAUF Company LTD, IPP Media, Shirika la Magazeti ya Serikali (TSN), Bravo Logistics na Lake Oil Company Limited, liliwasilisha michango yake juma lililopita.

 


FacebooktwittermailFacebooktwittermail