Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

RC TABORA: Limeni Alizeti Kwa Wingi

Na: Tiganya Vincent, RS-TABORA
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri ameagiza kuanzia msimu ujao wa kilimo kila mtu mwenye uwezo wa kufanyakazi ni lazima alime heka mbili za alizeti kwa ajili ya kuvutia wawekezaji kujenga Viwanda vya kusindika na kuzalisha mafuta hayo kuanza ujenzi mkoani humo.

Bw. Mwanri alitoa kauli hiyo jana wakati wa ufunguzi wa maonesho ya nanenane kwa Kanda ya mikoa ya Magharibi yaliyofanyika mkoani Tabora.

Alisema zao la alizeti katika mkoani  Tabora linastawi sana na ikiwa wakazi wake watalima kwa wingi Kampuni mbalimbali zitajitokeza kwa wingi kuja kujenga viwanda vya kuzalisha mafuta hayo.

Bw.Mwanri alisisitiza kuwa wawekezaji wengi wamekuwa wanashindwa kuja kujenga viwanda vya usindikaji wa mafuta hayo kwa sababu siku za nyuma zao hilo limekuwa halitiliwi mkazo na kufanya uzalishaji kuwa wa chini sana , lakini hivi sasa hiyo itakuwa ajenda ya Mkoa kama mkakati mojawapo wa kuwavutia watu kuja kujenga viwanda.

“Ndugu zangu Wakuu wote wa Wilaya na Wakurugenzi kuanzia sasa akili yetu na agenda yetu kubwa  iko katika kuhakikisha kuwa kila mkazi wa Tabora analima  heka mbili za alizeti kuanzia msimu ujao wa kilimo ili tuwe na malighafi nyingi kwa ajili ya kulisha viwanda vitakavyoanzishwa kwa mwaka mzima” alisema Mkuu huyo Mkoa.

Katika kutekeleza agizo hilo aliwaagiza Maafisa Ugani wote mkoani hapa kuhakikisha wanawatembelea wakulima vijijini kwa ajili ya kuwaelimisha juu ulimaji bora na mbegu bora za zao hilo kwa ajili kuwafanya wakulima kuanza  mara moja kilimo hicho pindi mvua za masika zitakapoanza.

Katika hatua nyingine aliwaagiza Wakurugenzi Watendaji wote na Maofisa Ugani wote kuhakikisha kuwa wanaanza wanawahimiza wakazi wa maeneo mbalimbali ya Mkoa huo kuanza kilimo cha zao la uwele , mtama, viazi na mihogo ili kukabiliana na tatizo la upungufu wa chakula kwa sababu ya  mvua kuendelea kunyesha chini ya kiwango.

Alisema tabia ya baadhi ya wananchi kuendelea kung’ang’ania mazao yanatumia miezi mingi kukomaa kusababisha wakazi hao kuendelea kukabiliwa na upungufu wa chakula wakati wakilima  mazao yanayostahimili ukame tatizo haliwezi kuwapata.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Nzega alisema kuwa wao tayari wameshaanza maandalizi kwa kuwa na shamba la mfano la heka 10 ambapo tayari wameshazalisha alizeti na kutoa mafuta.

Alisema kinachofuata ni kuongeza wigo wa kilimo hicho wa kuwashirikisha wananachi wengi kwa kuwaelimisha juu ya kilimo bora cha zao hilo ili waweze kuzalisha kwa wingi na kutoa fursa kwa wamiliki wa viwanda kupata malighafi ya kutoa kwa ajili ya uzalishaji mafuta.

Naye Mkazi wa Ipuli mkoani Tabora Juma Elia aliunga mkono agizo la Mkuu wa Mkoa wa Tabora la  kuhamasisha wakulima kuanza kulima alizeti ambalo ni rafiki na mazingira kwa sababu halihitaji kuni kukauka kama ilivyo tumbaku.

Aliongeza kuwa zao hilo litasaidia kutoa ajira kwa njia ya vijana kushiriki kilimo na wengine kuajiriwa katika viwanda vya kusindika mafuta ya alizeti vitakavyoanzishwa.

2 thoughts on “RC TABORA: Limeni Alizeti Kwa Wingi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama