Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Rc Kagera aiagiza TAKUKURU kufanya uhakiki wa ukusanyaji mapato Karagwe

Washiriki wakifuatilia mafunzo kutoka kwa mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo (hayupo pichani).

Na Nashon Kennedy, Bukoba

SERIKALI mkoani Kagera imeiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufanya uhakiki wa ukusanyaji wa mapato na matumizi ya  mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa maoato kwa halmashauri ya wilaya ya Karagwe, baada ya halmashauri hiyo kubainika kushindwa kutumia kikamilifu mifumo hiyo ambayo imewekwa kwa gharama kubwa ya fedha za walipa kodi.

Kauli hiyo imetolewa jana mjini Bukoba na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Diwani Athuman muda mfupi baada ya kufungua  mafunzo ya siku nne ya mfumo wa usimamizi wa fedha za umma wa epicor toleo la 10.2 ulioboreshwa ili kuwawezesha kubadilishana taarifa na Mfumo wa Mipango na bajeti, Mfumo  wa uhasibu na utoaji wa taarifa za fedha moja kwa moja kwenye vituo vya kutolea huduma (FFARS) kwa waweka hazina  na  maafisa wasimamizi wa fedha  mikoa ya Mara na Kigoma.

“Tumetuma timu maalum ya Mkoa ya Takukuru  kwenda wilayani Karagwe kufanya uhakiki wa ukusanyaji wa mapato, kama sehemu ya kuona matumizi ya mifumo hii inatumika vyema”, alisema.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Diwani Athuman akifungua rasmi mafunzo hayo. Picha zote na Nashon Kennedy, Bukoba.

Kufuatia hatua hiyo, Athuman amewaagiza Wakurugenzi watendaji wa halmashauri zote kutekeleza wajibu wao kikamilifu kwa kusimamia na kuitumia vizuri mifumo yote ya serikali iliyofungwa kwenye halmashauri zao ili kuleta ufanisi wa utendaji kazi, utoaji wa taarifa za serikali kwa wakati  na ukusanyaji wa mapato ya serikali.

“Iko mifumo mingi ya fedha katika halmashauri zetu ambayo imefungwa kwa gharama kubwa, lakini haitumiwi kwa kiwango kinachotakiwa cha kutuletea tija kwa kutoa huduma na shughuli mbalimbali”, alisema na kuongeza kuwa serikali itahakikisha kunakuwepo na matumizi sahihi ya mifumo ili kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato na utendaji kazi.

Alisema baadhi ya halmashauri nchini zimekuwa dhaifu katika kuitumia mifumo hiyo licha ya serikali na wafadhili kuingia gharama kubwa katika kuifunga, jambo ambalo alisema serikali italivalia njuga ili mifumo hiyo iweze kutumiwa vizuri.

“Kile kinachokusanywa na halmashauri zetu hakitumiki ipasavyo, unakuta halmshauri ina mashine za mfumo lakini zinaweka stoo na watu wanakusanya fedha na kuziweka mfukoni”, alifafanua.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera Diwani Athuman (wa tatu kutoka kushoto) waliokaa akiwa katika picha ya pamoja na washiriki kutoka mkoa wa Mara wa mafunzo ya siku ya nne ya mfumo wa Epicor yanayoendelea mjini Bukoba, baada ya kufungua rasmi mafunzo hayo jana.Alisema baadhi ya halmashauri nchini hazitumii mifumo ya fedha iliyopo na wakati huo huo wakishindwa kukusanya mapato na kufanya kazi kwa ufanisi na kuwataka kubadilika na kutumia mifumo hiyo kikamilifu ili kuboresha ufanisi na miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao ya kazi.
” Halmashauri nyingi zimekuwa zikilalamika kukusanya mapato kidogo kutokana na kutokuwa na mifumo, lakini ipo baadhi ya mifumo, ukiwemo mfumo wa Poss ambao hautumiki ipasavyo, na vifaa vya kusaidia mfumo huo vipo”, alisema.
Aliushukuru Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo katika sekta ya umma(PS3), serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto  kwa ufadhili wa michango yao ya hali na mali yaliyowezesha mafunzo hayo ya siku nne kufanyika na kutoa watalaam na raslimali kwa ajili ya mafunzo hayo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa PS3 Mkoa wa Kigoma Simon Mabagala alisema lengo la mafunzo hayo kwa watumishi hao ni kuwawezesha kuufahamu vyema mfumo wa Epicor 10.2 na mifumo mingine ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake, Mweka Hazina wa Halmashauri ya Kakonko mkoani Kigoma Mercy Swai alisema mafunzo hayo yamekuja kwa wakati muafaka na yatawaondolea changamoto za utendaji kazi wa kimfumo zilizokuwepo awali, ambapo kupitia mfumo wa Epicor 10.2 ambao unafanya kazi kwa kuunganishwa na mifumo mingine utawawezesha kufanya kazi kwa ufanisi kwa kutoa taarifa nzuri zinazofanana kwa mifumo yote.

Mfumo wa Epicor 10.2 ambao umeboreshwa yanayofanyika kwa mikoa ya Dodoma, Mwanza, Mtwara na Iringa  na mfumo wa mipango na bajeti na ule wa uhasibu na utoaji wa taarifa za fedha za vituo vya kutolea huduma (FFARS) yana lengo la kuwapa uelewa wa mabadiliko na maboresho yaliyofanyika kwenye mfumo  watumishi hao wa halmashauri nchini ili kufanya kazi zao kwa ufanisi.

 

 

 

 

 


FacebooktwittermailFacebooktwittermail