Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Rais Magufuli: Watanzania Tutembee Kifua Mbele, Tunaweza

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli, akihutubia wananchi mara baada ya kupokea Ndege mpya Aina ya Dreamliner 787-8, yenye uwezo wa kubeba Abiria 262, hafla hiyo ilifanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Kulia ni Spika wa Bunge Job Ndugai, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof.Palamagamba Kabudi na Kaimu Balozi wa Marekani, Dkt.Inmi Patterson..

Ndege Mpya Aina ya Dreamliner 787-8, yenye uwezo wa kubeba Abiria 262, ikimwagiwa maji (water salute) ikiwa ni ishara ya ndege mpya inapokuwa inapokelewa, hafla ya kuipokea ndege hiyo, ilifanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere Terminal 1Jijini Dar es Salaam .

Na Mwandishi Wetu-MAELEZO, Dar es Salaam

RAIS Dkt. John Magufuli amesema Tanzania itaendelea kutekeleza kwa kasi kubwa miradi ya maendeleo nchini kwa kuwa Serikali imeimarisha nidhamu katika usimamizi na matumizi ya rasilimali zilizopo pamoja na ukusanyaji wa kodi.

Akizungumza katika hafla ya upokeaji wa ndege mpya ya Serikali ya Boeing 787-8 Dreamliner katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere leo Jumamosi (Oktoba 26, 2019) Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli aliwataka Watanzania kujivunia na kuendelea kuiunga mkono Serikali yao kwa kuwa imedhamiria kuwaletea maendeleo ya kweli na ya haraka.

Rais Magufuli alisema Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla lina uwezo wa kufanya mambo makubwa  nay a haraka kutokana na kubarikiwa na rasilimali nyingi ikiwemo madini na hivyo Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kusimamia rasilimali hizo ili ziweze kuleta manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi walio wengi.

‘’Watanzania sisi ni matajiri tunaweza kufanya mambo makubwa na kununua vitu vizito kama ndege hizi, na tukiamua tunaweza kinachotakiwa sasa ni kuweza kuwa na matumizi mazuri ya fedha zinazopatikana kutokana na kodi tunazokusanya kutoka kwa wananchi wetu’’ alisema Rais Magufuli.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli akishuhudia makabidhiano ya ndege mpya Aina ya Dreamliner 787-8(Rubondo Island) kati ya Serikali na Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) yaliyofanywa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Ujenzi) Dkt.Leonard Chamuliho katika hafla ya kupokea ndege hiyo, ilifanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere Jijini Termianl 1 Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli akikata utepe kuzindua Ndege mpya Aina ya Dreamliner 787-8, yenye uwezo wa kubeba Abiria 262, hafla hiyo ilifanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere Terminal 1 Jijini Dar es Salaam, Wengine ni Kaimu Balozi wa Marekani, Dkt.Inmi Patterson na Viongozi wengine wa Serikali.

Aliongeza kuwa malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa sekta ya usafiri wa anga inapiga hatua kubwa ya maendeleo nchini na kwa kufanya hivyo Serikali imekusudia kuliwezesha Shirika la Ndege Nchini ATCL kuweza kutekeleza mipango na mikakati mbalimbali iliyojiwekea.

Akifafanua zaidi Rais Magufuli alisema ATCL kwa sasa ina jumla ya ndege 7 kati ya ndege 11 zilizopangwa kununuliwa na Serikali, hivyo aliitaka Menejimenti ya Shirika hilo kujipanga vizuri ili kuhakikisha kuwa linamudu ushindani wa kibiashara uliopo nchini ikiwemo kuimarisha mtandao wa usafirishaji abiria katika soko la ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli alisema ndege hiyo mpya ya Boeing 787-8 Dreamliner ni ndege kubwa ya kisasa yenye uwezo wa kubeba abiria 262 ikiwemo abiria 22 wa daraja la juu pamoja abiria 240 katika daraja la kawaida, hivyo kuitaka ATCL kuweka mipango na mikakati endelevu ya kuhakikisha itangaza vyema vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli, akiwa kwenye picha ya Pamoja na Kamati ya Bunge ya Miundombinu wakati wa mapokezi ya ndege mpya Aina ya Dreamliner 787-8, yenye uwezo wa kubeba Abiria 262, hafla iliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere Terminal 1 Jijini Dar es Salaam.

Ndege mpya Aina ya Dreamliner 787-8 yenye uwezo wa kubeba Abiria 262, iliyopewa Jina la Kisiwa cha Rubondo (Rubondo Island) kama inavyoonekana kwenye Picha katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.

‘ATCL hamna budi kujiendesha kibiashara na mnapaswa kutambua ndege hii ni mali ya Serikali na si ya ATCL hivyo na hilo linajionesha katika mkataba tuliosaini baina ya Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu Mkuu (Uchukuzi), hivyo hakikisheni mnafikia malengo yote tuliyowekeana’’ alisema Rais Magufuli.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dkt. Leonard Chamuriho alisema Shirika la ATCL limeendelea kutekeleza kwa mafanikio makubwa Mpango Mkakati wa Shirika hilo, ambapo sasa limeweza kufikia mafanikio ya asilimia 73 la usafirishaji wa abiria katika soko la ndani.

Aidha Dkt. Chamuriho anaongeza kuwa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya safari za abiria nje ya nchi, Shirika hilo pia limefanikiwa kuongeza idadi ya upokeaji wa shehena za mizigo kutoka nchini India na kufikia tani 178 na kuzisafirisha katika nchi mbalimbali ikiwemo Zambia.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli, akiwa kwenye picha ya Pamoja ya Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama katika Hafla ya Kupokea Ndege Mpya Aina ya Dreamliner 787-8, iliyopewa jina la Rubondo Island, hafla hiyo ilifanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere Termianl 1 Jijini Dar es Salaam.

Ndege Mpya Aina ya Dreamliner 787-8, iliyopewa jina la Rubondo Island inavyoonekana kwa Ndani, hafla ya kuipokea ndege hiyo iliongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli ilifanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Julius Nyerere Termianl 1 Jijini Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa Shirika hilo limepanga kushirikiana na Taaasisi ya Sekta Binafsi Nchini (TPSF) pamoja na Chemba ya Biashara,Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) kwa ajili ya kuweka nguvu na mkakati wa pamoja wa kuhakikisha kuwa inatanua mtandao wa usafirishaji wa shehena za mizigo nchini India.

Kuhusu soko la ndani, Dkt.Chamuriho aliongeza kuwa Shirika hilo limeweza kuongeza kituo cha usafirishaji wa abiria katika Kituo cha Mpanda Mkoani Rukwa pamoja na kupanga kuongeza idadi ya miruko ya ddege kutoka Dar es Salaam-Dodoma kufikia mara nne kwa siku ifikapo mwezi Desemba mwaka huu.

Naye Kaimu Balozi wa Marekani Nchini , Dkt. Imni Patterson aliipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kutokana na juhudi na hatua mbalimbali za makusudi inazochukua katika kuimarisha sekta ya usafiri wa anga kwani kwa kufanya hivyo kutaweza kutangaza sekta ya utalii pamoja na kuimarisha uchumi.

37 thoughts on “Rais Magufuli: Watanzania Tutembee Kifua Mbele, Tunaweza

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama