Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Rais Magufuli Ameahirisha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Akagua Ujenzi wa Barabara za Juu Ubungo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipita kukagua Maendeleo ya ujenzi katika sehemu ya gorofa ya pili ya barabara ya juu Ubungo Interchange ambayo iko katika hatua za mwisho kukamilika kwa ajili ya magari kuanza kupita. Mradi mzima wa Makutano hayo ya Ubungo umefikia asilimia 75.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na Mke wake Mama Janeth Magufuli wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Patrick Mfugale wakati akielezea Maendeleo ya ujenzi wa Barabara za Juu katika Makutano ya Ubungo, Ubungo Interchange jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameahirisha Mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka huu zilizopangwa kuzinduliwa tarehe 02 Aprili, 2020 huko Unguja, Zanzibar kwa lengo la kuchukua tahadhari ya kusambaa kwa virusi vya ugonjwa wa Corona (Covid-19) endapo utaingia hapa nchini.

Mhe. Rais Magufuli ametangaza maamuzi hayo leo asubuhi tarehe 16 Machi, 2020 alipokuwa akiwasalimu wananchi wa Ubungo, Mbezi Mwisho na Kibamba Jijini Dar es Salaam, wakati akikagua maendeleo ya upanuzi wa barabara na ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara za Morogoro, Sam Nujoma na Mandela eneo la Ubungo (Ubungo Interchange).

Pamoja na kuahirisha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Mhe. Rais Magufuli ameagiza fedha zilizoandaliwa kwa ajili ya mbio hizo zipelekwe Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ajili ya maandalizi ya kujiweka tayari endapo ugonjwa wa Corona utaingia hapa nchini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akikagua ujenzi wa Barabara za Juu katika Makutano ya Ubungo, Ubungo Interchange jijini Dar es Salaam.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amewasisitiza Watanzania wote kuendelea kuchukua tahadhari ya kuambukizwa virusi vya ugonjwa wa Corona kwa kuepuka misongamano, kutogusana, kunawa mikono kwa sabuni na maji yanayotiririka na kuzingatia maelekezo mengine ya wataalamu wa afya, lakini amesema ugonjwa huo bado haujaingia hapa nchini.

Katika ziara hiyo Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amekagua maendeleo ya upanuzi wa barabara ya Mwenge – Morocco yenye urefu wa kilometa 4.1 ambayo inajengwa njia 4 kwa gharama ya shilingi Bilioni 77.5 na ujenzi wa barabara za juu Ubungo ambao umefikia asilimia 70.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Wananchi waliokusanyika katika eneo la Mbezi Mwisho wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Morogoro katika eneo la Kimara -Kibaha ambapo upanuzi wake unaendelea na umefikia asilimia 70.

Ujenzi wa barabara za juu Ubungo unatarajiwa kukamilika kabla ya Desemba 2020 kwa gharama ya shilingi Bilioni 230 na unatarajiwa kusaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.

Mhe. Rais Magufuli pia amekagua maendeleo ya upanuzi wa barabara ya Kimara – Kibaha yenye urefu wa kilometa 19.2 ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 70 na inatarajiwa kukamilika Januari 2021 kwa gharama ya shilingi Bilioni 140.

Akiwa Mlandizi Mkoani Pwani Mhe. Rais Magufuli amesikiliza malalamiko ya wafanyabiashara ndogondogo wa eneo hilo walioondolewa kandokando mwa barabara na ameagiza wafanyabiashara hao warejee katika maeneo yao lakini wasifanyie biashara barabarani wala wasiwazuie wenye vibanda vya maduka kufanya biashara zao.

Mjini Chalinze, Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itahakikisha tatizo la maji katika Mji huo linamalizika baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa ambao unaendelea kutekelezwa.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Pwani

16 Machi, 2020

287 thoughts on “Rais Magufuli Ameahirisha Mbio za Mwenge wa Uhuru, Akagua Ujenzi wa Barabara za Juu Ubungo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama