Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Rais Magufuli Akutana na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akisalimiana na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia (WB) nchini B. Bella Bird aliyekutana na kufanya naye mazungumzo Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 9, 2018

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 09 Oktoba, 2018 amekutana na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia hapa nchini Bi. Bella Bird na kuzungumza nae kuhusu maendeleo ya miradi inayofadhiliwa na benki hiyo.

Baada ya mazungumzo hayo Bi. Bella Bird amesema miradi inayotekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia hapa nchini imefikia thamani ya shilingi Trilioni 10.186 na kwamba maendeleo ya miradi hiyo ni mazuri.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia (WB) nchini B. Bella Bird na ujumbe wake walipokutana na kuzungumza Ikulu jijini Dar es salaam leo Oktoba 9, 2018

Bi. Bella Bird ameongeza kuwa kwa sasa wanakamilisha maandalizi ya ufadhili wa miradi mingine inayohusu sekta ya elimu hasa elimu ya awali na sekondari, itakayogharimu shilingi Trilioni 1.357, na kwamba maandalizi hayo yatakamilika mwezi ujao.

“Kwahiyo nimekutana na Mhe. Rais Magufuli kuzungumzia maendeleo ya miradi hiyo na kwa ujumla maendeleo ni mazuri” amesema Bi. Bella Bird.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

09 Oktoba, 2018


FacebooktwittermailFacebooktwittermail