Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Rais Magufuli aadhimisha kumbukumbu ya Karume kwa kuzindua vituo vya polisi, nyumba za polisi na kujionea maonesho ya Polisi Jijini Arusha

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo na Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Simon Sirro wakifunua pazia kuashiria kufunguliwa rasmi kwa nyumba za makazi ya askari ya polisi za Naura zilizojengwa upya baada ya kuteketea kwa moto kwenye sherehe zilizofanyika jijini Arusha leo Aprili 7, 2018

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisaidiwa na viongozi wengine akikata utepe kuashiria kufunguliwa rasmi kwa nyumba za makazi ya askari ya polisi za Naura zilizojengwa upya baada ya kuteketea kwa moto kwenye sherehe zilizofanyika jijini Arusha leo Aprili 7, 2018

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 07 Aprili, 2018 ameungana na Watanzania wote kuadhimisha siku ya mmoja wa waasisi wa Taifa Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Kwanza wa Baraza la Mapinduzi kwa kuzindua kituo cha polisi, kufungua nyumba 31 za askari polisi na kushuhudia maonesho ya Polisi katika uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid Jijini la Arusha.

Kituo cha polisi cha watalii na wanadiplomasia kilichopo Naura, kituo cha polisi cha Muriet, na nyumba za 18 kati ya 31 za makazi ya polisi vimejengwa kwa mchango wa wafanyabiashara wa Mkoa wa Arusha  na Benki ya CRDB kwa gharama ya Shilingi Milioni 753, wakati nyumba za polisi 13 zimejengwa na Serikali kwa gharama ya Shilingi Milioni 250.

Mhe. Rais Magufuli aliagiza kujengwa kwa nyumba hizo baada ya kutokea ajali ya moto iliyosababisha nyumba 13 za makazi ya askari polisi na mali zao kuungua moto tarehe 27 Septemba, 2017.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akikata utepe akiwa na viongozi wengine pamoja na wadau waliosaidia ujenzi wa kituo maalumu cha Jeshi la Polisi cha Utalii na Diplomasia jijini Arusha kwenye sherehe zilizofanyika leo Aprili 7, 2018

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akifurahia jambo na baadhi ya familia za askari polisi baada ya kufungua rasmi nyumba za makazi ya askari ya polisi za Naura zilizojengwa upya baada ya kuteketea kwa moto kwenye sherehe zilizofanyika jijini Arusha leo Aprili 7, 2018

Katika kutekeleza agiza hilo Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo akaamua kuwashirikisha wafanyabiashara na benki ya CRDB kuchangia ujenzi huo na kufanikiwa kujenga nyumba nyingine 18 na vituo hivyo viwili vya polisi.

Pamoja na kuzindua miradi hiyo Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia maonesho ya Jeshi la Polisi ya kuzuia na kupambana na uhalifu yakiwemo kukabiliana na waandamanaji haramu, wezi, waporaji watumiao silaha na magaidi, yaliyofanyika katika uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid.

Akizungumza baada ya maonesho hayo Mhe. Rais Magufuli amesema Taifa litaendelea kumkumbuka Hayati Sheikh Abeid Amani Karume kwa juhudi zake za kujenga nchi ikiwemo kuwajengea makazi wananchi masikini kule Zanzibar na ametoa wito kwa Watanzania kumuenzi kwa kudumisha amani na kuchapa kazi.

Pamoja na kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Mrisho Gambo kwa jitihada zake za kuwaunganisha wadau na kisha kufanikiwa kujenga nyumba za askari na vituo vya polisi Mhe. Rais Magufuli ametoa Shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za askari polisi wa vyeo vya chini nchini, na amewaagiza viongozi wa mikoa yote kuwashirikisha wadau katika ujenzi huo kama ilivyofanyika mkoani Arusha ili kukabiliana na tatizo la askari kukosa nyumba za makazi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli akipokea saluti ya heshima baada ya kuwasili katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha kuadhimisha siku ya kumbukumbu ya miaka 44 ya kifo cha Rais wa kwanza wa Zanzibar Hayati Sheikh Abeid Amani Karume leo Aprili 7, 2018

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. John Pombe Magufuli akikagua gwaride la askari polisi katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha kuadhimisha siku ya kumbukumbu ya miaka 46 ya kifo cha Rais wa kwanza wa Zanzibar Hayati Sheikh Abeid Amani Karume leo Aprili 7, 2018

“Askari polisi mnafanya kazi kubwa sana ya kulinda raia na mali zao, natambua juhudi kubwa mnazofanya na napenda kuwashukuru sana, naomba Watanzania wote tuendelee kuliunga mkono Jeshi la Polisi.

“Wakati naingia madarakani kulikuwa na mauaji kila wakati, kule Kibiti pekee yake waliuawa watu 59 wakiwemo askari polisi 17 na raia 42, Jeshi la Polisi limefanya kazi kubwa na sasa mauaji yale yamedhibitiwa, ni lazima tulipongeze jeshi letu” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amekubali maombi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Simon Sirro la kuongezewa idadi ya askari na kupandishwa vyeo kwa maafisa wa polisi ambapo ameruhusu Jeshi la Polisi kuajiri askari wapya 1,500 kutoka Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na kumpelekea mapendekezo ya maafisa wanaostahili kupandishwa vyeo.

Mhe. Rais Magufuli amempongeza IGP Sirro kwa hatua ya kuwafukuza kazi askari polisi 458 waliokutwa na makosa ya kinidhamu na uadilifu kuanzia mwaka 2015 hadi sasa, na ametaka hatua hizo ziendelee kuchukuliwa dhidi ya askari wengine wanaokiuka maadili na taratibu za kazi ili kuondoa malalamiko kutoka kwa wananchi yakiwemo upokeaji rushwa na unyanyasaji raia kwa kuwabambikiza kesi.

Halikadhalika Mhe. Rais Magufuli amepiga marufuku askari, maafisa wa polisi na viongozi wengine wa Serikali kushiriki ufyekaji wa mashamba ya bangi na badala yake ametaka mashamba hayo yanapobainika yafyekwe na wanavijiji wenyewe waliohusika kuyalima.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Naibu Mawaziri, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, wabunge na wananchi.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Arusha

07 Aprili, 2018

34 thoughts on “Rais Magufuli aadhimisha kumbukumbu ya Karume kwa kuzindua vituo vya polisi, nyumba za polisi na kujionea maonesho ya Polisi Jijini Arusha

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *