Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Rais Dkt. Magufuli Awataka Mabalozi Kuleta Miradi ya Maendeleo Nchini

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza katika Kikao na Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali za nje Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali za nje mara baada ya kikao chao Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo inajengwa kwa fedha za Watanzania.

Mabalozi hao 43 ambao wapo hapa nchini tangu tarehe 13 Agosti, 2019 wametoa pongezi hizo leo tarehe 22 Agosti, 2019 walipokutana na kuzungumza na Mhe. Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Wametoa pongezi hizo baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa bwawa la Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 katika mto Rufiji, mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge railway) unaoanzia Dar es Salaam hadi Dodoma, jengo la 3 la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam Jijini Dar es Salaam, mradi wa ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara ya Morogoro na Sam Nujoma (Ubungo Interchange), mradi wa upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam, mradi wa usambazaji wa gesi (Taifa Gas), mradi wa udhibiti wa mawasiliano Tanzania na mradi wa ujenzi wa daraja la Tanzanite (New Selander Bridge) katika bahari ya Hindi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Brazil Emanuel Nchimbi mara baada ya Kikao na Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali za nje Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha na Waziri wa Mambo ya Nje Profesa Palamagamba Kabudi watano kutoka (kushoto), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Dkt. Damas Ndumbaro watano kutoka (kulia) pamoja na baadhi ya Mabalozi Wanawake wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali za nje Ikulu jijini Dar es Salaam

Kwa upande wa Zanzibar wametembelea mradi wa ujenzi wa jengo la biashara na makazi (shopping mall) eneo la Michenzani, mradi wa ujenzi wa jengo la 3 la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sheikh Abeid Amani Karume, mradi wa ujenzi wa nyumba za kisasa wa Fumba Wilaya ya Magharibi, mradi wa ujenzi wa barabara ya Kaskazini – Bububu – Mkokotoni na mradi wa ujenzi wa bandari ya mafuta na gesi katika eneo la Manga Pwani.

Mabalozi hao wameeleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na juhudi nyingine kubwa zinazofanywa na Serikali katika nyanja mbalimbali za huduma za jamii zimeleta heshima kwa nchi na machoni mwa Jumuiya ya Kimataifa, na kwamba zimedhihirisha kufikiwa kwa malengo ya Tanzania kuingia katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Pia wamempongeza kwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kipindi cha mwaka mmoja na wameahidi kuongoza vyema katika mikutano ya Mabalozi wa SADC katika nchi wanazowakilisha kwa kuzingatia mwelekeo ambao Mhe. Rais Magufuli ameutoa katika Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika tarehe 17-18 Agosti, 2019 Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kuwasilikiza Mabalozi hao, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza kwa kazi wanazozifanya katika nchi wanazoiwakilisha Tanzania na amewataka waendelee kutekeleza majukumu yao kizalendo na kwa kutanguliza maslahi ya Tanzania.

Pamoja na kueleza kuhusu hali ya uchumi wa nchi, juhudi za kuwapelekea maendeleo Watanzania na juhudi za kujenga uwezo wa kujitegemea, Mhe. Rais Magufuli amewataka Mabalozi hao kutafuta wawekezaji watakaowekeza katika miradi yenye manufaa hapa nchini.

“Nataka Mabalozi mtuletee miradi ya maendeleo, ifike mahali Balozi ujiulize kwa kuwa kwangu Balozi nimepeleka nini nyumbani? Nimewezesha kujengwa kiwanda? Kujengwa barabara? Kujenga daraja au jengo fulani?” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Mhe. Rais Magufuli amewasisitiza Mabalozi hao kuhakikisha wanasimamia na kufuatilia kwa karibu masuala wanayoamini yana manufaa kwa nchi ikiwemo uwekezaji na kwamba wasikubali kukwamishwa na viongozi ama wizara yoyote.

“Nataka muwe very aggressive, na ukiona mtu anakukwamisha mimi nipo niandikieni uone kama hatakwama yeye, mimi nataka kuona vitu sio maneno maneno” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Kuhusu changamoto mbalimbali walizomueleza, Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Mabalozi hao kuzishughulikia pale ambapo wao wenyewe wana uwezo na amemtaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kufanyia kazi taarifa wanazopelekewa na Mabalozi hao kwa wakati.

102 thoughts on “Rais Dkt. Magufuli Awataka Mabalozi Kuleta Miradi ya Maendeleo Nchini

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama