Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

PSSSF Yatumia Bilioni 122.9 Kulipa Kiinua Mgongo

Meneja Kiongozi Uhusiano na Elimu kwa Umma wa mfuko huo, Bi Eunice Chiume akiongea na Waandishi wa Habari leo Jijini Dodoma.

Na Mwandishi Wetu

Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) Umetumia Bilioni 122.9 kulipa kiinua mgongo wastaafu 2,650 kati ya June mosi hadi Julai 15, 2019.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dodoma, Meneja Kiongozi Uhusiano na Elimu kwa Umma wa mfuko huo, Bi Eunice Chiume amesema kuwa mfuko unaendelea kutekeleza jukumu la kuhakikisha kuwa wastaafu wanapata mafao yao kwa wakati mara wanapostaafu ili waweze kuendelea na shughuli za kujenga Taifa.

“ Jambo jingine la kujivunia ni kuwalipa wastaafu wetu pensheni ya mwezi kiasi cha shilingi Bilioni 92.7 huku wanufaika wa fedha hizo wakiwa 126,043 na tunaendelea kuhakikisha kuwa wanachama wetu wanapata huduma bora” Alisisitiza Chiume.

Akifafanua, amesema kuwa mfuko huo umeimarisha mifumo ya mawasiliano, hali inayowezesha wanachama kuwasiliana na mfuko huo wakati wowote wanapopata changamaoto au kutoa ushauri wao kuhusu huduma za PSSSF katika Ofisi zilizopo mikoani kwa upande wa Tanzania Bara na pia Visiwani.

Aliongeza kuwa mfuko huo unatoa fursa ya wanachama wake kuwasiliana nao kupitia namba za bure 080011005 na 0800110040 lengo likiwa kuimarisha mawasiliano kati ya wanachama na mfuko huo wa pensheni kwa watumishi wa umma.

Akizungumzia kuimarishwa kwa mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Bi Chiume amesema kuwa mfuko umeanza kutumia mfumo wa kielektroniki kuendesha shughuli zake ikiwemo kuhifadhi kumbukumbu mbalimbali; Mfumo huu husaidia kuongeza ufanisi, kupunguza matumizi ya karatasi na utunzaji wa uhakika wa kumbukumbu.

Mfumo mwingine ni ule wa Government Electronic Payment Gateway (GePG) hutumika katika ukusanyaji wa michango ya wanachama, mapato ya uwekezaji na mapato mengine. Faida za Mfumo huu zimegawanyika katika maeneo mawili, faida kwa mwajiri, ni pamoja na, kujifanyia tathmini ya michango inayoletwa PSSSF; kujitengenezea ankara za malipo; kutengeneza control number; kuweka hesabu sawa; kuweza kupata risiti kwa wakati; kulipa michango wakati wowote; kupunguza safari za kwenda kwenye ofisi za Mfuko kwa huduma mbalimbali.

Faida za mfumo huo kwa Mfuko ni pamoja na kuongeza uwazi, kuongeza ufanisi, kukusanya michango kwa wakati, mawasiliano rahisi na kutambua wanaowasilisha michango ya wanachama kwa wakati.

Baada ya Mifuko ya PPF, LAPF, GEPF na PSPF kuunganishwa na kuundwa kwa PSSSF tarehe 1/8/2019, serikali inafanya tathimini juu ya mafao ya uzazi, tathimini hiyo ikikamilika taarifa itatolewa kwa umma. Hata hivyo ofisi zote za Mfuko zinaendelea kupokea maombi ya kulipwa mafao ya uzazi kutoka kwa wanachama wa iliyokuwa PPF, LAPF, GEPF na PSPF, utaratibu wa malipo ya mafao ya uzazi kwa waliojifungua kabla ya kuazishwa kwa PSSSF wanalipwa kwa taratibu za Mifuko ya awali (PPF,LAPF,GEPF na PSPF); kwa wale ambao fomu zao zilishawasilishwa kwenye mifuko hiyo.

4 thoughts on “PSSSF Yatumia Bilioni 122.9 Kulipa Kiinua Mgongo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ev eşyası depolama