Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Pembejeo si Tatizo tena: Bodi ya Korosho

Na. Paschal Dotto, Georgina Misama -MAELEZO

Bodi ya korosho Tanzania imeongeza vituo vya ugawaji pembejeo ili kuharakisha usambazaji na kuhakikisha kila mkulima anapata pembejeo kwa wakati katika kudhibiti kuenea kwa magonjwa na wadudu wanaoshambulia zao la korosho.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam Mkaguzi Mwandamizi wa Ndani wa Bodi hiyo Bw. Christopher Mwaya alisema kuwa Bodi imeongeza uagizaji na usambazaji wa madawa ya salfa kutoka tani 15000 mwaka 2015-2016 mpaka kufikia tani 18000 mwaka 2017.

“Tumeongeza vituo vya usambazaji pembejeo kutoka vituo 2 hadi vituo 18 ili kuwafikia wakulima moja kwa moja na kwa wakati huko waliko pamoja na kuwapunguzia gharama za usafirishaji” alisema Bw. Christopher.

Bw. Mwaya alisema kuwa kamati za Wilaya chini ya Wakuu wa Wilaya zimepewa jukumu la kupanga na kusimamia mgawo kwa kufuata mwongozo uliotolewa na serikali kwa wakulima wenye mikorosho. Aidha, hadi sasa zaidi ya asilimia 71 ya madawa na salfa zimeshasambazwa kwa wakulima.

Akitolea ufafanuzi tuhuma za ucheleweshwaji wa madawa na viuatilifu Mwanasheria na Katibu wa Bodi hiyo Bibi. Ugumba Kilasa alisema kwamba, bado wapo ndani ya wakati kwa kuwa matumizi ya viuatilifu huanza mara tu korosho zinapotoa maua mwezi Juni. Hata hivyo kitaalamu Salfa hupulizwa awamu 5 kwa kupishana siku 21 kutoka awamu moja na nyingine.

Bi. Kilasa alisema kuwa kufikia Agosti 20, 2017 usambazaji wa pembejeo kwa wakulima wote kwa msimu mpya utakuwa umekamilika kwani tani zilizobaki kukamilisha usambazaji kwa wakulima wote tayari zimeingia bandarini na zipo katika taratibu za kutolewa ili kusambazwa.

“Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli ilitoa uamuzi wa kugawa bure madawa na pembejeo kwa  wakulima wa zao la korosho kwa lengo la kumwezesha mkulima na kumjenga kiuchumi ili awe na uwezo wa kujinunua mahitaji hayo kwa misimu inayofuata” alisema Bi Kilasa.

Aidha, Bi. Kilasa amewaasa wale wanaotoa maneno ya kuwavunja moyo wakulima wa zao hilo kuhusu kusambazwa kwa madawa na viuatilifu kwambi si huduma ya bure na kusema kwamba serikali imeamua kutoa madawa hayo kwa wakulima bure na kila mtu atapata kulingana na mgawo wa madawa hayo

Pia amewashauri wakulima kunyunyuzia dawa mara tatu katika mashamba yao na wakati mzuri wa kupiga madawa hayo ni pale korosho zikianza kutoa maua ili kuwezesha uzalishwaji mkubwa wa korosho.

Zao la korosho ni moja kati ya mazao makubwa nchini Tanzania ambapo takwimu za Benki kuu kwa mwaka 2016/17 zinaonesha zao hili linaongoza katika kuliingizia Taifa fedha za kigeni kwa mauzo ya Nje ya Nchi. Asilimia 80 ya zao hili hulimwa kusini mwa Tanzania katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Tunduru mkoa wa Ruvuma.

 

 

 

35 thoughts on “Pembejeo si Tatizo tena: Bodi ya Korosho

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *