Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Nyongo Awataka Wachimbaji Wadogo Kuwajibika

Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, akizungumza na wananchi na wachimbaji madini wadogo katika Mgodi wa Musasa uliopo Chato, akiwa katika ziara ya kazi inayoendelea Kanda ya Ziwa

Afisa Madini Mkazi wa Geita, Ally Maganga akitambulisha msafara wa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati), alipofika katika Machimbo ya Nyakafuru wilayani Mbogwe Mkoa wa Geita, akiwa katika ziara ya kazi inayoendelea Kanda ya Ziwa. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Martha Mkupasi.

Na Veronica Simba – Geita

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amewataka wachimbaji wadogo wa madini nchini, kufahamu wajibu wao na kuutekeleza kikamilifu ili waendeshe shughuli zao kwa amani na tija.

Aliyasema hayo Februari 26 mwaka huu, alipotembelea na kuzungumza na wachimbaji wadogo wa Lwamgasa, Bingwa, Musasa na Nyakafuru katika Wilaya za Mbogwe na Chato, Mkoa wa Geita, akiwa katika ziara ya kazi inayoendelea Kanda ya Ziwa.

“Msiishie kulalamika tu. Jifunzeni kuwajibika kikamilifu katika nafasi zenu ili kazi zenu zilete tija na kuwanufaisha ninyi wenyewe, jamii na Taifa kwa ujumla.”

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akiangalia Shimo la Uchimbaji katika Machimbo ya Madini ya Nyakafuru wilayani Mbogwe, akiwa katika ziara ya kazi inayoendelea Kanda ya Ziwa. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Martha Mkupasi.

Sehemu ya umati wa wananchi katika Machimbo ya Madini Bingwa, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani), wakati wa ziara yake inayoendelea Kanda ya Ziwa kukagua shughuli za madini.

Alisema kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya uongozi mahiri wa Rais John Magufuli, inawajali na kuwathamini sana wachimbaji wadogo lakini pia inawataka wawajibike ili mchango wao katika sekta husika uonekane.

Akifafanua zaidi, Naibu Waziri aliwataka wachimbaji hao kuhakikisha wanarasimisha shughuli zao kwa kuomba leseni ili wasajiliwe na kutambuliwa rasmi na Serikali, hivyo waweze kulipa kodi na tozo mbalimbali.

“Serikali inategemea kodi zenu ili iweze kutekeleza shughuli mbalimbali za maendeleo kwa Taifa ikiwemo kutoa elimu bure kama inavyofanyika sasa, kujenga miundombinu, kuwezesha utoaji wa huduma za afya na nyinginezo. Hivyo basi, ni lazima mlichukulie suala la uwajibikaji kwa umuhimu mkubwa,” alisisitiza.

Baadhi ya vitendea kazi katika Mgodi wa Musasa uliopo Chato, kama vilivyokutwa wakati wa ziara ya kazi ya Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani), Februari 26 mwaka huu.

Aidha, aliwasisitiza kuunda vikundi na kufanya shughuli zao ndani ya vikundi hivyo, ili iwe rahisi kwa Serikali kuwatambua na kuwapa huduma mbalimbali zitakazowasaidia kuboresha kazi zao.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) John Bina, aliwasisitiza wachimbaji hao kujali afya zao na kuzingatia suala la kutumia vizuri mapato yao ili wajiletee maendeleo.

Naibu Waziri Nyongo anaendelea na ziara ya kazi katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa.


FacebooktwittermailFacebooktwittermail