Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Naibu Waziri Nishati Awaonya Wakandarasi wa Miradi ya Umeme Vijijini

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (mwenye kilemba) akikata utepe kuashiria uwashaji rasmi wa umeme katika kijiji cha Ngazi, wilayani Lushoto, Machi 28, 2019 akiwa katika ziara ya kazi. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni, January Lugangika.

Na Veronica Simba – Lushoto

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewaonya wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini kuzingatia masharti yaliyowekwa na serikali hususani kutumia vifaa vya ndani ya nchi, na kwamba atakayeona hawezi kutekeleza masharti hayo, arudishe kazi hiyo kwa Serikali ili apewe mkandarasi mwingine.

Alitoa onyo hilo jana, Machi 28, 2019 katika kijiji cha Ngazi, wilayani Lushoto, Mkoa wa Tanga, wakati akizungumza na wananchi, kabla ya kuwasha rasmi umeme katika kijiji hicho.

“Kwanini muagize vifaa kama nguzo nje ya nchi wakati sisi bado miti tunayo na mingine imepandwa kwa makusudio hayo?”

Alisisitiza kwamba wakandarasi wanaochelewesha kazi kwa visingizio vya namna hiyo waache mara moja kwani sababu hizo hazina mashiko.

Naibu Waziri alilazimika kutoa onyo hilo kufuatia kazi duni ya mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza (REA III – I) wilayani Lushoto, ambao ni muunganiko wa kampuni za Njarita, Aguila na Radi.

Sehemu ya umati wa wanafunzi wa Shule ya Msingi na wa Sekondari Ngazi, wilayani Lushoto, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani), alipokuwa akizungumza katika hafla ya uwashaji rasmi wa umeme kijijini Ngazi, Machi 28, 2019. Naibu Waziri aliwasha umeme katika Shule ya Sekondari Ngazi akiwa katika ziara ya kazi na kuwasisitiza wanafunzi wautumie umeme kuboresha kiwango chao cha elimu.

Alipohojiwa kuhusu suala hilo, Mkandarasi husika alitoa utetezi kwamba mojawapo ya sababu zilizofanya acheleweshe kazi ni agizo la serikali linalowataka wakandarasi kutoagiza vifaa nje ya nchi, badala yake watumie vifaa vya ndani ya nchi.

Akijibu utetezi wa mkandarasi husika, Naibu Waziri alimtaka kujitathmini kuona kama anakidhi vigezo kwani wenzake wanaotekeleza miradi ya aina hiyo sehemu mbalimbali za nchi wanafanya vizuri.

“Tumewasha vijiji zaidi ya 1,900 katika Mradi wa REA III na karibu kila Mkoa na Wilaya, vijiji vimewashwa. Wewe uliomba kazi hii na unashindwa. Inakuwaje wenzako wanaweza?

Akifafanua zaidi, Naibu Waziri alisema kuwa kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais John Magufuli, matarajio ni kuwa, ifikapo Juni 2021, vijiji vyote vilivyokuwa havina umeme tangu serikali husika iingie madarakani, ambavyo vilikuwa takribani 7,873; viwe vimepata umeme.

Alisema, wakati mwingine baadhi ya wakandarasi wanarudisha nyuma jitihada hizo ndiyo maana Serikali ikaunda kamati mbalimbali za usimamizi. Aliwataja wasimamizi wa miradi ya REA kuwa wanatoka ngazi ya Wizara, REA, Meneja Tathmini wa Mkoa, mafundi mchundo wa Wilaya pamoja na wasimamizi wa Kanda.

“Hata hivyo, mwisho wa siku, msimamizi mkuu ni Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya wakishirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama za maeneo yao,” alibainisha.

Katika hatua nyingine, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ngazi wilayani Lushoto, kabla ya kuwasha rasmi umeme katika kijiji hicho, Naibu Waziri alisisitiza kuwa gharama ya kuunganishiwa umeme kwa wananchi wa vijijini ni shilingi 27,000 tu.

Aidha, alitoa rai kwa walimu wa Shule ya Sekondari Ngazi iliyopo wilayani humo, ambayo ndiyo aliyoiwashia umeme; kuhakikisha wanautumia umeme waliounganishiwa kuboresha kiwango cha elimu shuleni hapo.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini wilayani Lushoto, Meneja wa TANESCO wilayani humo, Mhandisi Kasim Rajabu alimweleza Naibu Waziri kuwa, mradi ulianza kutekelezwa Julai 2018 na mkataba wake ni wa miaka miwili, ambapo hadi sasa umekamilika kwa kiwango cha asilimia 30.

Alisema, mradi unahusisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33, yenye urefu wa kilomita 33.6, usimikaji wa mashine umba 61 na ujenzi wa njia ndogo za umeme zenye jumla ya urefu wa kilomita 112.

Nyingine ni uunganishaji wa wateja wapya wa awali 1,338 ambapo wateja wa matumizi ya kawaida ni 1,300 na wale wa viwanda vidogo vidogo ni 38.


FacebooktwittermailFacebooktwittermail