Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Ikupa Ahimiza Vyama Vya Watu Wenye Ulemavu Kushirikiana na Serikali

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu, Mhe. Stella Ikupa ameviasa Vyama vya Watu wenye Ulemavu nchini kuhakikisha wanashirikiana na Serikali katika kuendeleza ustawi wa Watu wenye Ulemavu.

Naibu Waziri Ikupa ameyasema hayo alipofanya ziara Mkoani Dodoma kukagua utekelezaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu ndani ya mkoa huo, ambapo alikutana na viongozi Mkoa na Vyama vya Watu wenye Ulemavu.

Mhe. Ikupa alieleza kuwa ushirikiano baina ya Serikali na vyama vya watu wenye ulemavu ni muhimu katika kuhakisha haki na masilahi ya watu wenye ulemavu yanalidwa kwa kuzingatia Sera, Sheria na Miongozo mbalimbali.

“Serikali imeendelea kuchukua hatua na kutekeleza jukumu lake la kuhamasisha na kuwalinda watu wenye ulemavu nchini kwa kuhakikisha haki za kundi hilo maalumu zinatekelezwa,” alisema Ikupa

Aidha, alisisitiza uongozi wa Mkoa kuhakikisha unahusisha mahitaji maalumu ya wenye ulemavu katika bajeti wanazozitenga, kutoa elimu na taarifa juu ya upatikanaji wa dawa, mafuta ya watu wenye ualbino na vifaa saidizi, na uundwaji wa kamati za kuhudumia wenye ulemavu.

Aliongezea kuwa, ni vyema Maafisa Maendeleo ya Jamii pamoja na maafisa ustawi wa jamii wakahakikisha wanawasaidia watu wenye ulemavu wanapokabiliana na changamoto kwenye uandikaji wa maandiko ya kuomba mikopo.

“Unakuta kikundi cha watu wenye ulemavu wanakuwa wabunifu na wanawazo zuri la kuanzisha mradi au biashara lakini wanakumbana na changamoto ya kuaandaa andiko la miradi yao na hivyo kuwafanya wakate tamaa mapema,” alisema Ikupa

Pia, aliwasii Maafisa Ustawi wa Jamii kuwa na takwimu sahihi za idadi ya watu wenye ulemavu na kuendelea kuweka mifumo mizuri ya kutunza taarifa hizo.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Bw. Edward Mpogolo aliunga mkono na kuyapokea maelekezo yote ya Naibu Waziri na kumhakikishia kuwa Mkoa wa Dodoma utakuwa mstari wa mbele katika kutekeleza maagizo aliyoyatoa.

 “Tutafanya kazi kwa ushirikiano mzuri na Vyama vya Watu wenye Ulemavu ili kuangalia namna bora ya kuwahudumia kwa kuzingatia mahitaji yao,” alisema Mpogolo.

Nae Katibu wa SHIVYAWATA Mkoa wa Dodoma, Bw. Justus Ng’wantalima alimpongeza Naibu Waziri kwa jitihada ambazo amekuwa akizifanya katika kutetea Watu wenye Ulemavu.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri Ikupa, alitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Chama cha Walemavu Sulungai kinachojishughulisha na ushonaji wa viatu vya wazi (kobasi) na utengenezaji wa majiko. Vilevile Mhe. Ikupa alitembelea shule ya Viziwi iliyopo Jijini Dodoma.

71 thoughts on “Ikupa Ahimiza Vyama Vya Watu Wenye Ulemavu Kushirikiana na Serikali

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *