Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Juma akisoma kipeperushi katika Banda la Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba katika Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea jijini Dodoma tarehe 27 Januari 2022.
Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Katika kuhakikisha mlundikano wa mashauri ya migogoro ya ardhi unapungua nchini, Msajili wa Mabaraza ya Ardhi, Stela Tullo ameelekeza Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kwenda kusikiliza mashauri katika wilaya nyingine ambazo hazina Wenyeviti.
Akizungumza katika maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea jijini Dodoma Stela alisema, lengo ni kutatua migogoro ya ardhi kwa wakati na haraka sambamba na kusogeza huduma karibu na wananchi.
Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya, Stella Tullo (kushoto) akimfafanua jambo mmoja wa wananchi waliotembelea banda la Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba katika Maonesho ya Wiki ya Sheria yanayoendelea jijini Dodoma.
“Katika kusogeza huduma karibu na wananchi tumeamua kusogezea huduma karibu wananchi ambapo tumejiwekea mikakati na kuelekeza Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya kwenda wilaya nyingine ambazo hazina wenyeviti kusikiliza mashauri ya wananchi na siyo wananchi kuwafuata wenyeviti walipo”. Alisema Stella.